webnovel

chapter 7

Tulya anaendelea kuifuata sauti ya kalimba akipita kwenye vichaka kuelekea sehemu ilipo,anasogea karibu na Mahali ilipo lakini hamuoni mtu anayepiga, anajishauri asogee karibu zaidi Ili aone,akili nyingine inamwambia akisogea karibu nzagamba atamuona na yeye hataki aonekane.

Anaendelea kujitahidi kuangalia lakini anashtushwa na sauti ya sinde iliyokuwa inamuita,anageuka nakuanza kukimbia kurudi upande alikokuwa anachota maji.Nzagamba aliyekuwa juu ya mti anasikia sauti ya mtu ikiita anageuka na kuona mtu akiishia hakufatilia anaendelea na kupiga kalimba yake.

Tulya anafika na kumkuta sinde "ulienda wapi wewe ukaacha vibuyu hapa?" anauliza sinde baada ya kumuona "msalani,umemaliza kuchota hicho" anajibu huku akitengeneza ngata yake tayari kujitwisha kibuyu" ungenisubiri nifike au unataka watu wabebe vibuyu" tulya Anacheka "nani abebe kibuyu,kingine mi sijui ulikuwa inachukua mda gani kuongea na laazizi wako aliyetoroka Kambi kukuona wewe tu ndo ningevumilia tu kama sio kujikojolea ni nini" wanajitwisha nakuanza kuondoka "subiri siku Moja vibuyu viibiwe uanze kubeba mtungi ndo utaona namaanisha nini wewe si mbishi" anaonya sinde "acha hizo niambie kwanza alikuwa anasemaje shemeji" "alikuwa kanikimbuka hatujaonana mda mrefu" "ndio katoroka mchana huu hakamatwi" tulya anauliza huku masikio yake yakianza kufuatilia mziki wa nzagamba uliokuwa unaishia kwa mbali moyo wake ukijiuliza ni namna gani maisha ya nzagamba yalivyo magumu mda wote kukaa peke yake.

Akiendelea kutembea sinde anasimama ghafla tulya aliyekuwa anamfuata nyuma anajigonga kwenye mgongoni kwa sinde kibuyu kinayumba anataka kukidaka lakini alishachelewa kuanguka chini na maji kumwagika "mama yangu mzazi kibuyu changu mama ataniua ,unatembeaje wewe?"anang'aka tulya akiendelea kukusanya mabaki ya kibuyu yaliyobakia akitamani kukiunganisha kuzuia Balaa lakini anajua fika kuwa haiwezekani "kwani huna macho wewe ona umenilowanisha"anashtuliwa na sauti ya kiume tulya ananyanyua uso na kumwangalia aliyeongea,anasimama "utakuwa hujaona vizuri kijana sijakumwagia maji kibuyu kimeanguka na maji yakamwagika uwe unanyoosha maelezo vizuri" tulya aliyekuwa kavurugwa akiwaza kubebe mtungi jinsi ulivyomzito Kila siku alikuwa Yuko kwenye kiwango Cha kumaliza hasira kwa mtu yeyote "unasemaje wewe" anang'aka yule mwanaume uso ukimjaa hasira,tulya anaisikia sauti na kuhisi kama anaijua lakini hakukumbuka aliisikia wapi "samahani kaka manumbu ni makosa yangu nilisimama ghafla nikamfanya ajigonge mgongoni kwangu"anaongea sinde akitaja jina la manumbu kuepusha matatizo zaidi kwani anamjua tulya haachagi Mambo nusu nusu.

Baada ya tulya kusikia jina la manumbu na kufananisha sauti anajua kweli ni yeye kwani siku ile hakuikariri sura alikuwa na hasira vilivile kulikuwa ni usiku.Tulya anarudi nyuma kwenye mgongo wa sinde mikono yake ikichezea ngata yake.manumbu anamwangalia sinde,alikuwa anamjua kupitia kaka zake " haya nendeni" "asante" anaitikia sinde akimshika mkono tulya nakuanza kuondoka "subiri kidogo" wanashtuliwa na sauti ya manumbu na wote miguu Yao ikasimama huku wakitetemeka.

manumbu anarudi hadi pale walipo nakuanza kumkagua tulya kuanzia juu mpaka chini,tulya anajaribu kuficha hasira yake asingekuwa amesikia habari za manumbu angemlipukia vibaya sana kwa kumwangalia namna ile lakini aliamua kutulia Ili asizue balaa zaidi " huyu nani sinde"anauliza manumbu macho yake yakiondoka kwa tulya na kwenda kwa sinde "ni binamu yangu mtoto wa shangazi ni mgeni" sinde anaongea huku rohoni akiomba manumbu asimkumbuke tulya kutokana na sakata la siku ile usiku lakini maombi yake yote yalianguka hatua chache tu baada ya kutoka kinywani mwake "aaa! ndugu yako asiyekuwa na akili nzuri" anaongea manumbu kuwaonyesha kuwa anakumbuka tukio la siku chache zilizopita.

Tulya anaona miguu yake ikimuisha nguvu,kijasho chembamba kinamtoka lakini anajikakamua kumuonyesha kuwa hamuogopi manumbu "msamehe tu siku ile hakuwa vizuri" sinde anaomba msamaha akijua fika kuwa tulya hakuwa hata na wazo la kufanya hivyo,tulya anatamani kuongea lakini anatulia.

Manumbu anarudisha tena macho kwa tulya akimwangalia kama awali "nendeni ila siku nyingine ukinikosea adabu usidhani kama nitakuonea huruma sawa Leo nakuacha sababu najua wewe ni mgeni na kwa ajili ya sinde"anaongea manumbu na kuanza kuondoka.Sinde na tulya wanachia pumzi zao zote walizokuwa wamezibana

"yaani huyu na Mimi hatuendani kabisa Kila tukikutana ni majanga tu damu yangu haimpendi hata kidogo" anashtuliwa na kibao Cha sinde begani kwake " aaah!unaniumiza umenipigia nini?" tulya anauliza huku akijishika alipopigwa na sinde macho yake yakienda kwa sinde na kule alikoondoka manumbu " hivi utajifunza lini kuudhibiti mdomo wako huo,ile kauli ya mdomo huponza kichwa huijui wewe" sinde anaongea nakuanza kutembea tulya nae anamfuata " makosa ya nani haya yote usingesimama ghafla Mimi nisingejigonga na kuangusha kibuyu hata hivyo ungewahi na kutaja jina la manumbu Ili Mimi nimuone wewe ukatulia tu,ona Sasa nimevunja kibuyu kama ulivyotaka na Mimi nitaanza kutumia mtungi" analalamika tulya akiendelea kutembea "Mimi nilishtuka kumuona,na sikuongea sababu nilijua unamjua"

" nitamjuaje wakati siku ile ilikuwa ni usiku na purukushani lile hata sikumwangalia vizuri,kwani ana matatizo gani Kila wakati Yuko kwenye hali mbaya tu,au ndo kutaka kuonyesha madaraka yake" anaongea tulya akitupa mikono " ndo alivyo huyo na tatizo la lindiwe limeongezea kabisa"

maneno ya sinde yanamfanya tulya kuhamishia akili yake kwake " mke wake anashida gani" anauliza tulya kwa shauku "watu wanasema hazai wameoana miaka miwili Sasa mkewe hajazaa wala kushika mimba wenzake wote Wana watoto kasoro yeye tu hata zinge na kilinge waliooa mwishoni wake zao wanamimba hiyo inamvuruga zaidi,ila usije ukagusa hapo atakuua ni mkali kama nini" tulya anatikisa ulimi "tsi tsi,nilijua wanaishi vizuri baada ya waliomfanyia mwenzao kumbe Kila mzimu na mbuyu wake" anaongea tulya akiwasikitikia.

"Vipi mbona uko hivyo umevunja kibuyu"anauliza runde baada ya kumuona tulya bila kibuyu Cha maji "tulikutana na manumbu wakapamiana kibuyu kikaanguka" sinde anajibu akitua kibuyu chake " hajagomba kweli maana hachelewi yule" anauliza runde akiwa na wasiwasi "hajagomba sana" sinde anajibu akielekea ndani "vizuri,fanyeni mbebe huo unga mpeleke kwa wifi yenu mke wa kilinge mkamsalimie hatujaenda mda mrefu" mke wa kilinge anayekaribia kujifungua alienda kwao kujifungua " yule nae anapenda tu kukaa kwao alienda mapema sana anatusumbua tu,wenzake wanajifungulia tu kwa wakwe zao yeye akaamua kwenda kwao" analalama sinde akiinama na kuosha mtungi wa maji "acha kuongea fanya haraka muondoke,ukiolewa na wewe utaona tu ukweni sio sawa na nyumbani" runde anaongea na kuelekea ndani.

"mbona sijamuona kaka kilinge na zinge tangu Jana?" anauliza tulya akikaa kwenye jiwe lililo chini ya mti "wameenda kujiandaa kuelekea porini kuwinda kwa ajili ya sherehe ya matambiki" "zitakuwa lini?" "siku nne zijazo" anaongea sinde akimimina maji ya kwenye kibuyu akiyahamishia kwenye mtungi " nyama zitakuwa nyingi siku hiyo ee" tulya anauliza akisimama na kwenda alipo sinde " ndio hasa za kuchoma,unapenda nyama wewe?" sinde anamtania " hasa za kuchoma,kwani wewe hupendi" wote wanacheka.

Siku ya matambiko ikawadia na Kila mtu katika Kijiji Cha rumo alikuwa kwenye shamrashamra za sherehe vijana na mabinti wakijiremba na kujichora michoro mbalimbali katika miili Yao,makundi ya vijana wawindaji walioenda porini walikuwa wamesharudi wakiwa na nyama kwa ajili ya sherehe.

sherehe za matambiko ni sherehe za kimala na desturi ambako watu wote huchinja wanyama na kufanya tambiko wakiomba mizimu na miungu Yao kwa ulinzi na na kushukuru kwa Mambo mbalimbali mazuri yaliyowapata kwa mwaka mzima.

Pembeni ya Kijiji nyumbani kwa nzagamba, nzagamba anatoka akiwa amejiandaa kwenda kwenye sherehe anatoka na kumkuta mama yake akishona ukiri "mama mbona bado upo hapo"anamuuliza mama yake akisimama na kushika kiuno "niende wapi" anauliza bibi sumbo akiendelea na ukili wake pasipo kumtia machoni kijana wake "mama Leo umesahau kama ni siku ya tambiko" anamkumbusha mama yake akihisi kasahau lakini akijua haiwezekani " watu wote wameshaelekea huko wewe bado upo hapa mbuzi wetu nani atamsimamia" bibi sumbo anatupa ukiri wake chini na kumwangalia kijana wake "mbuzi yupi na unataka nikafanye tambiko kwa kuiambia nini mizimu, ni miaka mingapi Sasa nafanya matambiko wanachokifanya ni kula nyama tu hawafanyi chochote ninachokitaka nyama yenyewe wanataka ya mbuzi hivi wanajua kubadilisha mbuzi ni ghari kiasi gani?" nzagamba anamwangalia mama yake kwa mshangao aliyekuwa akiongea kwa hasira "mama hujabadilisha mbuzi" anamuuliza "kwa ajili ya nani wao hawafanyi majukumu Yao na Mimi sifanyi yangu tumemalizana na mwaka unaokuja nitafanya hivyohivyo" bibi sumbo anaushika ukiri wake na kuanza kushona tena "huoni kama utaikasirisha mizimu" nzagamba anamwangalia mama yake kwa kutokuamini kuwa anagombana na mizimu "kwani yenyewe tu ndio inajua kukasirika Mimi pia najua,maisha ya mwanangu hayaeleweki na bado nitoke nikawachinjie mbuzi kwa kazi gani waliofanya?" nzagamba anaanza kuondoka akijua kubishana na mama yake akiamua kitu hakuzai matunda "utafute na mchumba huko" bibi sumbo anamsindikiza mwanae lakini nzagamba hata hakugeuka kumwangalia,hiyo maada imeshakuwa mziki maishani mwake Kila siku anawaza tu ni lini mama yake atakubaliana na Hali halisi.

Nyumbani kwa Mzee Shana,runde na mumewe Mzee Shana wakiwa wanaondoka sinde na tulya wakiwasindikiza kwa macho "mje mkimaliza kazi hizo nilizo waambia kwanza bado mapema hata sherehe hazijachangamka" runde anawasisitiza, "muwahi kabla watu hawajamaliza nyama zote,tusimfanye tulya akalia"anamtania Mzee Shana akiondoka."tufanye haraka tuende" tulya anaongea akimsukuma sinde wakielekea ndani "baba kasema tuende mchana wewe unataka tuwende Sasa hivi" "Nina hamu ya kuona sherehe zenu huku zinaendaje" "haya tufanye haraka" Wanaingia ndani.

Kwenye mti mkubwa nje kidogo ya Kijiji Cha rumo sherehe zikiendelea watu wote wakiwa wamesimama na mganga mkuu wa Kijiji akiwa Mbele akiwa ameshika kifimbo chenye manyoya ya mkia wa Ng'ombe mkono wake wa kushoto akiwa ameshikilia kipeo chenye pombe akichovya unyoya kwenye kipeo na kukitikisa huku na kule akimwanga ile pombe,watu wote wakiwa kimya wakimwangalia kwa mkini na mlio wa ngoma ukipigwa kwa sauti ya chini. anamaliza na kuchukua damu za wanyama kwenye kipeo na kuanza kufanya vile vile baada ya kumaliza kitendo hicho anachukua ile pombe anakunywa na kuitema pande zote nne za Dunia "enyi mizimu ya mshariki,mizimu ya magharibi,mizimu ya kusini,mizimu ya kaskazini tumekuja kuwarudishia shukrani zetu kwenu kwa kutulinda mwaka wote huu na kututimzia mahitaji yetu,pokeeni sadaka zetu hizi zilizopo Mbele yenu" anachukua damu ile ya kwenye kipeo na kuimwaga kwa kuzunguka mti huo mkubwa unaosadikika kuwa ni Mahali mizimu inapoishi baada ya kumaliza kitendo hicho anakunywa pombe na kuitema tena pande zote nne ngoma zinapigwa pamoja na panda linalia kuashiria maombi kukamilika na watu wote wanapiga kelele za kushangilia wakiimba na kucheza.

Baada ya sherehe za matambiko kuisha,shamrashamra zinaamia Kijijini kwenye uwanja mkubwa wa maonyesho mbalimbali ya ngoma na mengine ambayo huudhuriwa na vijana,tulya na sinde wanafika wakiwa wamejiremba na kujichora michoro usoni kwao na kufunga midundiko kiunoni huku miguuni wasisahau kuvaa njuga zao tayari kwa kucheza "nyama ziko wapi" anauliza tulya baada ya kuangaza huku na kule asione chakula "zipo kule nyuma ya nyumba twende tukale kwanza halafu tuje kucheza" wanaondoka na kuzunguka upande wa pili ambako walikuwepo vijana na watu wenye umri wa makamo wakichoma nyama na kupika kwa ajili ya sherehe.

wanaoenda na kuchukua nyama choma wanatafuta kivuli Cha mti kilichokuwa na gogo wanakaa na kuanza kula,baada ya kumaliza wanarudi sehemu ya burudani na kuanza kuangalia.

Kinaingia kikundi Cha sarakasi na tulya anamuona manumbu akiwa kiongozi pamoja na zinge,baada ya hapo kinakuja kikundi kingine Cha ngoma na kiongozi wao akiwa kilinge "kilinge na zinge wako vikundi tofauti" tulya anauliza pasipo kumwangalia sinde "ndio, zinge kiongozi wake ni manumbu" "kama namuona kaka yangu asivyopenda fujo kukaa na wale wapenda fujo na walevi" anaongea tulya akibetua midomo yake akitikisa kichwa kwa masikitiko kumwonea huruma zinge "yule mdada ni mzuri na kapendeza kweli" tulya anaongea baada ya kuangalia upande wa pili na kuona kikundi Cha wadada watatu wakija upande wao.

Sinde anageuka na kuangalia alikokuwa anaangalia tulya anashtuka lakini kabla hajajibu wale wadada watatu wanafika walipo "habari zenu" anasalimia sinde kwa heshima tulya kuona hivyo na yeye anasalimia

" ndio wewe" anauliza yule dada tulya aliyesema ni mrembo akimwangalia tulya juu chini,tulya anashtuka "ehh" na kuitika kwa sababu hakuelewa "nasikia wewe ndio uliyekuwa unajitupa kwa mume wangu,nataka nikupe onyo sipendi kuchangia vitu usije ukajichanganye kabisa" anaongea yule dada na kuondoka huku wakimwangalia tulya kwa dharau.

Tulya aliyekuwa bado akizungusha akili yake kujua nini kinaendelea anarudi na kuwaona wale wadada wakiondoka "subiri da.." kabala hajamaliza sinde anamshika mkono "achana nao hata ukjieleza hawakuelewi wale" "kwani kimetokea nini mbona sijaelewa" anauliza tulya akiangalia kule walikokuwa wanaelekea wale wadada " lindiwe huyo mke wa manumbu atakuwa alipata habari za Siku ile kwenye ngoma amekuja kulinda himaya yake" tulya anaweka mdomo Wake kwa herufu ya o kwamba kaelewa "huyo na mume wake wote wameendana kweli wanajiona wao ndo wao,simtaki huyo mumewe hata kwa ng'ombe mia itakuwa Bure" anaongea tulya akinyanyua kichwa chake kuelekea kule alikopotelea lindiwe na marafiki zake na kumfanya sinde acheke "achana nao hao,twende tukacheze ni mda wa watu wote kucheza" sinde anamvuta mkono na kuelekea sehemu ya kucheza ngoma.