webnovel

Chapter 58

Nzagamba anageuka kuangalia anakoonyesha kidole Lingo,macho yanamtoka kwa mshtuko na mapigo yake ya moyo yanaanza kwenda mbio.Anameza funda la mate na linaanguka kooni kwake kama jiwe limetupwa kwenye shimo.Macho yake yanaendelea kumwangalia Tulya namna alivyovaa.Nyeele zake kichwani zikiwa zimesukwa mabutu mawili na Kisha kuzungushiwa shanga zilizoning'inia katika paji la uso wake.Uso wake ukiwa umechorwa vidoti vyeusi na vyeupe vinavyomwongezea mvuto wake wa asili.

Shingo yake ikiwa imezungukwa na shanga zilizotengenezwa kwa duara isiyo kubwa sana kiasi Cha kufunika mifupa ya shingo yake pia isimkabe shingo yake.Kitambaa kidogo kilichofunika kifua chake na kutoa uhuru wa kutosha kwa maziwa yake ambayo Kila akitembea yanatikisika.Tumbo na mgongo wake vikiwa wazi,kitovuni kwake ikiwa inaning'inia shanga nyembamba iliyotokea katikati ya mgongo na kuishia kitovuni.Kiunoni akiwa amevaa shanga nyingi zilizorundikana akiziacha mlegezo.Taratibu sura ya Nzagamba iliyokuwa na mshtuko mwanzo Sasa imeanza kujikunja kama mgonjwa anayekosa radha ya chakula Kila baada ya sekunde.

Anamwangalia sketi aliyovaa ni fupi iliyofika juu ya magoti na katikati ya mapaja,miguuni akiwa amevaa viatu vya kufunga kamba mpaka magotini.Vifundo vya miguu yake vikiwa vimefunikwa na njuga.Macho ya Nzagamba yanaangaza huku na kule anaona wanaume wote waki mwangalia mke wake.Amevaa nini yule anajiuliza utadhani hamuoni.Anakunja ngumi kwa hasira,Taya zake zikiwa zimegandana kwa kujaribu kuzuia hasira zilizokuwa zinamtuma kwenda kumchukua Tulya na kumpelekea nyumbani kwake na kumfungia ndani mtu yeyote asimuone akiwa vile.

" huyo ni Tulya?" anashtushwa na sauti ya Kilinge lakini macho yake yanaendelea kumwangalia mtu anayefanya watu wamuone kama yeye ndio chakula Cha sherehe ya harusi ya Sinde na Tinde.Marafiki zake wanamwangalia Nzagamba ambaye kwa wakati huu nywele zake zinakaribia kufuka Moshi unaotokana na moto unaowaka ndani yake.Lakini Kuna mtu asiyejua alama za nyakati katika kundi lao anaamua kuharibu zaidi.

" kapendeza sana,shemejii...aaah" anaongea Mkita akimwita Tulya kwa nguvu lakini anagugumia kwa maumivu baada ya kupigwa na Lingo ubavuni." nini?" anauliza akigeuka na kumkazia macho Lingo lakini mambo tayari yalishaharibika kwani Tulya anageuka na kuangalia walipo akiwapungia mkono na tabasamu juu.Malimbe nae anafanya hivyo baada ya kumuona mumewe na marafiki zake.

Wengine wote wanarudisha tabasamu kama salamu isipokuwa Nzagamba ambaye macho yake yalikuwa kwa Tulya.Macho Yao yanakutana na tabasamu lililokuwa usoni kwake kuanza kufifia baada ya kuona sura ya Nzagamba na wakati akitafakari kujua nini kimempata Nzagamba anageuka na kuangalia kwingine.' kapatwa na nini yule?" anajiuliza Tulya baada ya kumuona Nzagamba amekasirika.Amemkasirikia yeye au? lakini hawajaonana tangu juzi!anawaza.

" chakula hicho" anashtuliwa na mtu anayeongea nyuma yake anageuka kuangalia chakula kinachowekwa kwenye kundi alilokuja kukaa ambako Malimbe tayari alishakaa na baada ya kuona nyama choma mawazo ya Nzagamba yanamtoka kwa sasa alishe tumbo lake kwanza Kisha akaupakache mziki unamuita masikioni kwake.Anakaaa nakuanza kula.

"kapendeza sana shemejii yangu" Mkita anaendelea kutabasamu jino kwa jino wakati mwenye mke sura ikiwa imejikunja kama kalamba ndimu."kwa nini hukumwambia mkeo avae vile?" Lingo anamuuliza

" natamani sana" anaongea Mkita mkono wake ukienda kushika shavu lake akianza kuota namna mke wake atakavyopendeza akivalia mavazi ya ngoma.

" lakini Tausi atakufa akitoka mlango wa nyumba tu kwa aibu.Ni bora kuwa nae mzima bila kuvalia mavazi ya ngoma kuliko apende lakini awe marehemu" anamalizia Mkita akivuta na kutoa pumzi kwa nguvu kuonyesha kuwa tatizo lake halina utatuzi anaoutaka na ameshakubaliana na hali halisi.

"ndio maana nawaambia shemejii yangu kapendeza hembu muoneni huyo mke wa Nsio" anaongea Mkita akianza kucheka.Marafiki zake wanageuka na kumuona Mbula aliyevaa sketi fupi kuliko ya Tulya na kufanya miguu yake mirefu na myembamba kuwa kama kachunwa nyama zote na kubakishiwa mifupa.

" Yule mwanamke Kila siku nikimuona huwa haachi kunichekesha,we subiri aanze kucheza utaona,angepewa na kiuno ingekuwa shida" anazidi kucheka Mkita na kuwafanya wenzake nao kucheka isipokuwa Nzagamba ambaye macho yake yanatoka kwa Mbula na kwenda kwa Tulya aliyekuwa anacheka kwa kitu walichokisema wenzake.

Tabasamu Lake likiangazi kama nyota na mwezi wakati wa giza kinene na kufanya anga kuonekana maridadi.

'Hii ni sherehe Nzagamba,' anajifokea mwenyewe akijaribu kujizuia Kila akimwangalia Tulya na namna wanaume wenzake ambao hawatoi macho yake kwake.Sio kama Tulya ni mwanamke pekee aliyevaa nguo fupi,Kuna wanawake waliovaa nguo fupi zaidi kama Mbula.Wengi huvaa nguo fupi zaidi siku za sherehe kuwarahisishia kucheza kutokana na sketi zao ndefu kuwa nzito.Lakini Nzagamba anaona sketi zinazomfika magotini mke wake ndio zinamfaa zaidi kuliko hii ya kuonyesha mapaja yake njee na kufanya Kila mwanaume atamani kuyashika.

Mapaja ambayo yeye mwenyewe hajawahi kuyaona na Leo anachangia na watu wengine.Afadhali angekuwa kama mke wa Mkita anawaza Nzagamba lakini anajua fika kuwa mke wake ni mwanamke huru asiyefungamana na upande wowote.Na kwa kuwa ni sherehe anaamua kuvumilia kwa masaa machache tu ya mateso na Kisha Kila kitu kitakuwa sawa.Akili yake inamwambia hivyo lakini mwonekano wake ni tofauti kabisa na alichokubaliana nacho.

" kwa nini umelegeza shanga zako?" mwanamke Mmoja anamuuliza Tulya wakati wakiendelea kula." Mimi mwenyewe nilitaka kuuliza" anaongezea mwanamke mwingine.

" hizi?" anauliza Tulya akiangalia shanga zake kiunoni " utaona kazi yake baadae" anaongea Tulya akitabasamu." nilimuuliza akanijibu hivyo hivyo" anaongezea Malimbe akiendelea kuvuta nyama kwa meno akizitenganisha na mfupa. Watu wanamaliza kula na michezo mbali mbali inaanza watu wakifurahia sherehe.

"Mnaondoka?" Tulya anamuuliza Sinde baada ya kuwaona wamesimama " ndio,Tinde kasema kachoka akapumzike" Sinde anamjibu akimwangalia mume wake anayeongea na marafiki zake." Nadhani sitakuona ukicheza" Sinde anajibu akijisikia vibaya kwani bado alitaka kukaa na kuona sherehe yake vizuri.

"mmmh,Naona mumeo hataki kuchelewa" Tulya anaongea kwa sauti ya chini akitabasamu huku akimpiga bega Sinde kwa bega lake.

" kasema kachoka sana,amekuwa akipitiliza mno"Sinde anamjibu " kwa mtu aliyetoka safari ya siku nne au tuseme Tano kasori na bado akakimbilia kukuona kweli kachoka,kachoka kukaa mbali na wewe na ushahidi tutauona kesho asubuhi" Tulya anacheka."Tuondoke" Sinde anamsikia Tinde akimwita anamuaga Tulya na kuondoka.

" mapema sana" anaongea Tulya akiangalia jua ambalo ndio kwanza linaanza kuzama.Anaamua kuachana na Wana ndoa wapya na kuanza kumtafuta Nzagamba. baada ya kuzunguka huku na kule pasipo mafanikio anaamua kwenda kuangalia burudani ikiendelea.

Upande wa pili Nzagamba na marafiki zake wanawasili makusanyiko kwani walikuwa wameondoka kiza kikiwa kimeingia na makusanyiko yakiwa yanatawaliwa na mwanga wa miale ya moto.Wanashangaa kuona watu wakiwa wameweka duara wakishangilia na ngoma zikiendelea kurindima." Kuna nini?" anauliza Kilinge wakianza kupita katikati ya mkusanyiko wapate kuona kinachowafurahisha watu." oh,oh,oh hii kubwa kuliko" anaongea Lingo akiangalia katikati ya watu penye mduara

" Yuko vizuri" anasikika mwanaume pembeni Yao akiongea." Nzagamba ana bahati sana,hembu ona kiuno hicho" anasikika mwingine."Anacheza kama Hana mfupa" mwingine anaongea.

" shemu Yuko vizuri,watakuwa wanashindana,hembu mwone mke wa Nsio huwa hakubali kushindwa" anaongea Mkita akicheka peke yake kwani katika Hali hii yeye tu ndio alikuwa anaona kiburudusho wengine wanageuka na kumwangalia.Nzagamba macho yake yameganda kwa Tulya aliyevuta macho ya watazamaji.

Tulya yupo katikati ya ulingo akicheza.Sasa utaelewa kwa nini alivaa shanga zake mlegezo.Kila akizungusha kiuno shanga nazo zinazunguka Kisha anazitupa juu zinaenda mpaka karibu na kitovu zinakutana na ile aliyoifunga katikati ya mgogo zinazunguka na kurudi tena kiunoni.Mchezo unaenda kwa jina la cheza na shanga.Mchezo maarufu katika himaya ya wafugaji na ni watu wachache wanaoweza kuucheza Tulya akiwa ni miongoni mwa wasichana wanaoujua mchezo huu.

Kati ya wasichana waliotoka mwali kwa miaka miwili mfululizo yeye pekee ndio aliweza kujua kucheza na Sasa anautumia hapa himaya ya Mpuli kwa wawindaji ambao hawajawahi kuuona kabisa.

" wooo" watu wanashangilia wengine wakipiga makofi na miluzi baada ya Tulya kuinama akiitupa shanga zake na kurudisha kiunoni inaganda kama imebanwa na ulimbo.Mchezo ulioanza kama mashindano kati ya Tulya na Mbula wakitafuta nani anajua kucheza zaidi.Na sasa Mbula anaonekana kama ndege aliyeangukia kwenye povu la pombe na mbawa zake zimelowa lakini bado anajaribu kupaa.

" woooooo" watu wanazidi kushangilia pasipokujua Kuna mtu anatamani kuvunja Taya zao wote.Tulya anatupa kichwa nyuma akikaa kama anataka kuangukia mgongo lakini bado hafiki chini na kuanza kuchezeaha maziwa yake.Wakati Anacheza anamuona mtu anakuja " Nzagamba?!" na kabla hajakaa vizuri Nzagamba anamvuta na kuanza kuondoka nae.Uvumilivu wake umekatika kabisa.