webnovel

chapter 54

Anapiga hatua haraka mpaka alipoweka kibuyu chake Cha maziwa na kuelekea waliposimama wenzake anaona wanaume waliobeba nyama na wengine ngozi za wanyama Moja kwa Moja anajua wale ni wapokeaji.Macho yake yanaangalia pembeni yake na kumuona Lindiwe akitetemeka kama jani wakati wa kipupwe." uko sawa?" anamuuliza na Lindiwe anaitikia kwa kichwa.

Vigelegele vya wanawake vinamrudisha kundini na kuona wanaume wakiingia wakiwa wamebeba silaha zao mikuki,mishale,pinde na sime zao kiunoni.Ukilinganisha na kundi la kwanza lililofika Hawa hawaonyeshi kuchoka sana.Macho yake yanaenda kwa kakayake Zinge na wenzake waliokuwa wakicheka kutokana na mazungumzo Yao isipokuwa Zinge.Ntali anamfuata anampokea na kumpatia kibuyu Cha maji,Zinge anakunywa akimuuliza mkewe anaendeleaje naye anamjibu vizuri akimpa pole ya safari.

" shikamoo kaka Zinge" Tulya anamsalimia Zinge akiangalia nyuma yake ambako msafara ulikuwa bado unaingia." Marahaba,una habari nzuri leo Tulya" anamwambia.

" ehh?!" Tulya anaitikia na macho yake yaliyokuwa yanaangaza huku na kule kutua kwa mtu aliyekuwa anamtafuta kwa mda mrefu.Mwendo wake kama shujaa aliyerudi vitani na ushindi, nywele zake kichwani zikiwa zimevurugika zaidi,rubega yake anayoifunga siku zote ikiwa haipo ikiacha kifua chake wazi kikionyesha misuli yake inayojua kifuani hapo ndio nyumbani kwao.

Uso wake ukiwa makini kusikiliza kitu ambacho anakiongea Kilinge.Miguu yake inaanza kupiga hatua kuelekea kule aliko yenyewe kama imevutwa na sumaku.

Kabla hajafika alipo anamuona amesimama macho yake yakianza kuangaza huku na kule, Tulya anajua kuwa anamtafuta yeye na haikumchukua mda kumuona katikati ya kundi la watu.Macho Yao yanakutana na anaanza kupiga hatua kuelekea alipo wapate kukutana njiani.

" Tulya" anaita Nzagamba kwa sauti ya chini ambayo kutokana na makelele ya watu anaisikia yeye tu.Mapigo yake ya moyo yanatulia kwa sekunde kabla ya kuendelea na safari.Na kwao wawili Dunia ilikuwa kama haipo na wapo wao tu wawili na hawajali kwani wanajitosheleza hawahitaji nyongeza.

" uko sawa?umeumia? wapi?lete nione" Bashasha zote zinayeyuka kwa mfululizo wa maswali ya Tulya akimgeuza geuza kumkagua.

" Tulya,subiri..." anajaribu kuongea lakini anakatishwa.

" nisubiri nini kama umeumia unahitaji kutibiwa haraka" anaendelea kubwabwaja pasipo kujali kuwa walikuwa wanavuta umakini wa watu wote kwao.

" maji" anamsikia Malimbe akimpa kibuyu Cha maji Kilinge na yeye ndio anashtuka"aaah! maji" anachukua kibuyu chake kumpatia anakumbuka kuwa amebeba maziwa.Anampatia kibuyu chake Malimbe,naye anakidaka kabla hakijatua chini.

" aaah" anashtuka Kilinge baada ya kunyang'anywa kibuyu Cha maji kabla hakijafika mdomoni mwake." kunywa" na Sasa kilikuwa mikononi kwa Nzagamba.

" Tulya..."

" kunywa maji,kukaa siku tano na kiu sio kitu rahisi"

Watu wanaowazunguka wanabaki wakiwaangalia midomo ikiwa wazi nzi anaweza kunywa maji ya ulimi akaondoka wao hawana hata habari, Kilinge ni miongoni mwao ambaye haamini kama dada yake amemwacha afe kwa kiu amuokoe mume wake kwanza.

" kama huwezi kunywa maji chukua maziwa haya hapa" anaongea Tulya baada ya kumuona Nzagamba akimwangalia tu pasipo kunywa maji.Kibuyu kilichokuwa mikononi mwa Malimbe kina hama tena na kwenda mikononi mwa Tulya.Anampatia Nzagamba lakini mikono yake imeshajaa " mpe hicho kaka Kilinge" anamwambia.

"aaah" anaguna baada ya kuhisi maumivu kichwani anageuka na kumuona Kilinge ndie aliyempiga.

" ndio,Mimi ni kaka yako,unaninyang'anya vipi maji na kumpatia mumeo"

" ehh?" akili ndio inarudi anageuka na kuona watu wote wakiwaangalia macho yake makubwa yanapita huku na kule na Kisha kurudi kwa Nzagamba anayeendelea kumwangalia pasipo kusema kitu Wala kufanya chochote.

Sasa anamwangalia ndio anagundua ni kiasi gani alimkumbuka,macho yake,sauti yake na Kila kitu hasa harufu yake ya udongo.Nzagamba alikuwa anaziona siku mwaka huko porini na alifanya Kila kitu arude kuja kuona macho hayo makubwa.safari yake ya siku nyingi hatimae imemfikia tamati na Sasa Yuko nyumbani.

" kwani ulikuwa hujanywa?" anamuuliza Kilinge.

" khaaa!" Kilinge anaitikia kama anamuuliza unamaanisha au lakini Mkita aliyekuwa pembeni Yao anaona kivutio na kuangua kicheko." mshanyang'anywa huyo" anacheka Mkita.

" vipi shemu tukupatie habari nzuri?" anaongea Lingo baada ya kumaliza kunywa maji aliyopewa na mkewe.

" hiyo isubiri kwanza" anajibu Kilinge ambaye hajaamini alichofanyiwa na Tulya.

" chukua" Nzagamba anampatia kibuyu Cha maji Kilinge kumaliza mzozo.

" wewe hujanywa!" Tulya anadakia akijaribu kudaka kibuyu amrudishie Nzagamba.

" mumeo umeona hajanywa ila Mimi hukuona?!" anauliza Kilinge.

" wewe umezoea.."

" inatosha Tulya Niko sawa" Nzagamba anamjibu tabasam likija mdomoni kwake kuona ni namna gani mkewe anavyomjali.

" vipi nyumbani wazima wote,chakula mlipata?" anamsikia Mkita akimuuliza mkewe na Tulya kuzungusha macho asimuamini chizi huyu

" nakuaminia mke wangu" Mkita anamsifia mke wake baada ya kuitikia kwa sauti ndogo na Tausi anaangalia chini kwa aibu.

kati ya wanandoa wa ajabu ni wale pale anawaza Tulya.

"chukua" anashtuliwa na sauti ya Nzagamba anageuka na kuona ameshikilia ngozi anaipokea." ni ngozi ya swala,niliemuwinda kwa mshale" anaongea Nzagamba na macho ya Tulya yaliyokuwa yakiangalia ngozi kukimbia usoni kwa Nzagamba yakikaribia kung'oka hiki ni kitu ambacho hakukitarajia.

" hongera shemu,umeleta bahati maishani mwa rafiki yetu kipenzi" anaongea Mkita akija kusimama pembeni ya Tulya na kuongezea kwa sauti ya chini " na asante kwa kuijali familia yangu" maneno ambayo Tulya hakuyasikia kwani mshtuko ulikuwa ni mkubwa.Machozi yanamlenga kwenye macho yake makubwa.

Watu wote wanashangaa baada ya kusikia kuwa Nzagamba amewinda.Tulya pasipokujali umati wa watu anamkumbatia machozi yakimwaguka " hongera kazi nzuri Nzagamba" anamwambia.Nzagamba anaganda akitaka kumtoa lakini Tulya anamganda kama ruba.Anasikia watu wakinong'ona kuwa Hana aibu kufanya kitu kama kile mbele za watu lakini Tulya alikuwa na furaha sana kujali maneno ya watu na mazingira na siku zote huwa hajali likija suala la Nzagamba.

Watu wanakuja na kumpatia Nzagamba hongera wengi wao wakiwa hawaamini.Na habari ikawa ni ya Nzagamba tu.Nzagamba na wenzake wanakaa na wake zao wanawatengea chakula nakuanza kula.Kwa mbali Tulya anamuona Manumbu akiwa kama kamezeshwa mzizi wa mtu wa mlungulila sura ikiwa imejikunja zaidi ya ngozi iliyokauka pasipo kunyooshwa.Lakini Tulya alikuwa katika furaha sana na hakuwa na muda wa kujali nani anawaza nini.

Baada ya kula watu wanatawanyika Kila mtu akiisubiri kwa hamu siku ya kesho kwa ajili ya sherehe ya vijana waliotoka lindo na kesho kutwa yake kwa ajili ya harusi ya Sinde.Na furaha inazidi zaidi kwani sherehe zote zitakuwa na chakula Cha kutosha.

Nzagamba na Tulya wanarudi nyumbani kwao na Bibi sumbo ni mwenye furaha zaidi kumuona kijana wake baada ya siku nyingi tena akirudi na habari njema.Tulya ana andaa maji ya moto na kumwekea Nzagamba akaoge.

" vipi mbona wima?" Nzagamba anamuuliza baada ya kumuona amesimama.Tulya anakohoa kidogo " inabidi niondoke" Nzagamba anakunja uso kwa kutokumuelewa.

" inabidi niende kwa mjomba,nalala huko kwa sababu ya maandalizi ya harusi" anamjibu na Nzagamba anamuelewa.

" unaenda mwenyewe?" anamuuliza.

" ndio,hakuna tatizo" anajibu.

" haya wasalimie " anamjibu na kupita chumbani.

Tulya anatoka nje na kuona kiza kimezidi anasimama na kufikiria kupiga nduki ndefu mpaka kwa mzee Nshana lakini kwa pumzi zake bado anaona atapelea kufika pasipo kupumzika.

" twende" anamsikia Nzagamba akiongea nyuma yake na kumpita kutangulia mbele.

" umechoka kapumzike tu" anaongea Tulya akimkimbilia nyuma.Kwa mtu muoga una mdomo kweli anawaza Nzagamba.Moyoni akiwa hajafurahishwa na kitendo Cha mkewe kuondoka kwani alikuwa anahitaji kuwa nae karibu kufidia siku ambazo hajamuona ikiwezekana afanye naye mambo yanayomsumbua kichwani kwake kwa siku nyingi lakini anaona atavumilia kwa siku mbili hizi sio mbali sana.

Mbali na walipo katika himaya ya Mpuli katika kasri la mtemi Limbo zinasikika nyayo za mtu akitembea kwa haraka mwanga wa mwale wa moto mkononi mwake ukimwongoza kuona vizuri anakoelekea.Anafika na kusimama katika mlango wa nyumba Moja kati ya nyingi zinazoizunguka boma ya mtemi na kuita.

" bwana,bwana" anasubiri mda na anapoona haitikiwi anaita tena " bwana,bwana"

" Kuna nini usiku huu?" inasikika sauti iliyotoka usingizini.

" wakuu wanakuita bwana wangu"

" wanataka nini tena? kwani hukuwapelekea sadaka Yao?" inauliza sauti ikionyesha kukereka.

" nilipeleka mkuu,ila wamesema ni muhimu" anasisitiza aliyesimama nje.

" Kila siku wanasema hivyo hivyo wakishapata sadaka zao" mlango unafunguliwa na anatoka kijana mwenye umri kati ya miaka thelathini na tano akitengeneza rubega yake vizuri.Sura yake ikionyesha dhahiri hajapenda usumbufu anaoupata lakini inamlazimu kutekeleza.

" wanataka nini?" anauliza akifunga mlango wake kwa nyuma nakuanza kutembea mtu aliyesimama nje anamfuata kwa nyuma lakini bado akihakikisha mwale wa moto unasafirisha mwanga mbele ya bwana wake Ili apate kuona vizuri anakoelekea.

" sijui bwana,ila wameitisha kikao Cha ghafla na mtemi mkuu pia ameitwa" anajibu.

"mmmh,basi itakuwa ni muhimu mpaka wamemwita na huyo kikongwe" anajibu mwanaume akiendelea kutembea.