webnovel

chapter 53

Tulya anawasili makusanyiko na kukuta wanawake wengine wenye kiherehere kama yeye au kumzidi wameshafika.Anaangalia huku na kule lakini haoni watu alioambiwa wamefika.Si walisema wamefika? anajiuliza akiendelea kupepesa macho yake lakini anachoona ni wanawake wenzake tu waliosimama makundi makundi wakiongea na wengine wakiwa wamekaa.miale ya moto iliyowashwa kuzunguka eneo ikiangaza na kufanya isiwe vigumu zaidi kumuona mwenzio.

Tulya anawafuata kundi la kina mama waliosimama karibu yake na kuwasalimia.

" habari ya jioni,shikamooni" wote wanamwitikia,wakubwa wanachukua heshima Yao na wadogo wanarudisha salamu yake." nilisikia wamesema wamefika mbona siwaoni?" anauliza macho yake makubwa yakiwakagua wote akitegemea jibu kwa Mmoja wao." yule alikuwa ni mtoa taarifa tu,alikuja kutuarifu kuwa wanakaribia hivyo inabidi tuwasubiri kidogo mpaka watakapo wasili" anamjibu Mmoja wapo.Tulya anakunja uso kwani hakutegemea hilo " bado wako mbali sana au?" anauliza sauti yake ikiwa Haina uvumilivu " hatujui,lakini kwa sababu wameenda kupokelewa haitachukua Lisaa" anajibu mwanamke mwingine akimkagua Tulya uso wake ukionyesha kuwa Tulya anampotezea muda wake isitoshe alikuwa anapewa taarifa za yaliojiri kijijini ambazo zilikuwa hazijamfikia.

Tulya Sasa anaelewa kwa nini wifi zake walikuwa wanakuja wakitembea kama kinyonga.Angejua kama watachelewa hivyo angekimbia nyumbani kumwandalia mumewe chakula Cha moto na maji ya moto angeacha jikoni anawaza Tulya lakini tayari alishafika na hawezi kuondoka tena.

" ni mke wa Nzagamba huyo" mtiririko wa mawazo yake yanakatika baada ya kusikia jina la mumewe likitajwa na wanawake aliowauliza." ndio maana hajui kinachotokea baada ya watu kwenda mawindoni" anajibu mwanamke mwingine mwenye umri kama wa mama yake.Tulya anawaangalia wakiendelea kumsema utadhani yeye hayupo pale.

"Atajulia wapi wakati mumewe hajawahi kwenda kuwinda na hata Leo sijui kama hajarudi na sime na uchovu" anaongea mwanamke wa awali mwenye kiherehere Cha habari mpya kijijini.Tulya anamwangalia na kuona atakuwa anamzidi umri kidogo kwani mwanamke huyu anaonekana kakomaa kidogo kama anashindaga kwenye shamba la kuvuna ndago anawaza Tulya moyoni sura ikianza kujikunja kwani inaonekana Kuna mtu anampango wa kumharibia jioni yake.

" kaja mapema akijua leo atapumzika kula ndege" anaongezea mwanamke mwingine na wote wanacheka." na haitoki kwa jasho la mumewe itakuwa ya mgao" anaongezea mwanamke aliyekomaa kama Tulya anavyomwita " Hawa wanawake..." anatulia kidogo na kuvuta pumzi kutuliza hasira." Tulia Tulya usifanye fujo Nzagamba anarudi Leo" anajisemea kwa sauti ya chini asitake mumewe kufika akute amevuruga mapokezi yake na hiyo ndio bahati Yao anawaza Tulya akiendelea kuwakazia macho.

"Aaaah" anashtuka baada mtu kumshika bega anageuka na kuwaona wifi zake Malimbe na Ntali." tulikwambia tusubiri" Ntali anamwambia akitabasamu " mwache,atakuwa anaona siku tano pasipo Nzagamba ni kama mwaka,mimi siku Moja tu nilikuwaga naona mwaka" anaongezea Malimbe na wote wanacheka.Tulya anatabasamu kwa aibu.

" dada?!" anaita Ntali na kundi la wanawake waliokuwa wanamsema wanageuka.

" Ntali" mwanamke aliyekomaa anamwita mke wa Zinge na kumfanya Tulya kushangaa kwani anawajua dada zake Ntali wote huyu katoka wapi?

Ntali anasogea karibu Yao na kuanza kuwasalimia " ni mtoto wa baba yake mkubwa" anamsikia Malimbe na macho yake kugeuka haraka na kumwangalia " ndio maana tabia zao zinatofautiana" anaongea Tulya macho yake yakirudi kwa Ntali na dada yake. "na wewe umemuona?" Malimbe anamuuliza." watu kama Hawa wapo kama boga na kibuyu huwezi kuchanganya kupika" Malimbe anacheka.

Tulya anatoa macho kwa ndugu wawili wanaoendelea kusabahiana na macho yake kwenda kwa mtoto mgongoni kwa Malimbe.

" amelala mweke vizuri,mjombaangu" anamwambia na kumwita mtoto mjomba kwani amerithishwa jina la Nshana Babu yake.

" unajua kama kaolewa na mzee kama baba yake" Malimbe anaongea akiinama kumtengeneza mtoto vizuri.

" nani?" Tulya anauliza ambaye alishasahau habari waliokuwa wanaizungumzia awali.

" dada yako hapo" Malimbe anamjibu akitupa kichwa chake kwa ishara.Macho ya Tulya kidogo yaanguke kwa mshtuko.

" usiniambie!kwani vijana waliisha?" anamuuliza akijisogeza karibu Ili asipitwe na neno hata Moja.

" jeuri yake hakuna aliyetaka kumuoa,alikuwa anampenda Malala lakini akamkosa.." anatulia kidogo baada ya kuona Tulya akimwangalia kwa kumuuliza Malala ni nani." ni kijana Mmoja hivi huwezi kumjua we jua hivyo tu,Malala akamwoa rafiki yake,roho ikamuuma Muli.Akavumilia lakini ukapita mda hajaolewa na umri ulikuwa unaenda,ikabidi aolewe na baba yake Malala kama mke mdogo wa nne" Tulya anabaki mdomo wazi.

" huyo mdada hapo pembeni ndio mke wa Malala na alikuwa rafiki yake lakini Sasa ni mtu na mkamwana wake,na kiherehere chote hicho kamsindikiza mwenzie Kuja kumpokea mumewe wakati wake kazeeka Yuko nyumbani,atakuwa huwa anajisikia vibaya kwani tangu aolewe hajawahi kuja kumpokea mumewe mawindoni kwa sababu haendi tena na muda wote hujifanya kama yeye ndio mke wa Malala na sio mwenzake.

Nadhani anataka amfanye Malala ajute kwa kujifanya yeye Bora kuliko mwenzie, we subiri utaona wakifika" anaongea Malimbe akimalizia" ingekuwa Mimi hata nisingemruhusu amsogelee mume wangu lakini yule nae yupo kama mjinga mda wot...." anaacha kuongea baada ya kumsikia Tulya akicheka kwa nguvu na kufanya watu wote waache kuongea wageuke kuwaangalia.

Tulya anacheka na kushika tumbo lake Malimbe na wengine wakimshangaa na kujiuliza ni nini kilichomfurahisha.

" uko sawa?" Malimbe anamuuliza lakini Tulya anaendelea kucheka akifanya watu wazidi kumshangaa na muda huo Lindiwe aliyefika mda mrefu na alikuwa anamtafuta anafanikiwa kumuona anamvuta mkono Tausi na kuja kusimama alipo Tulya.

" unacheka nini?" Lindiwe anauliza lakini Tulya anaendelea kucheka na baada ya muda anaacha kucheka mkono wake ukifuta machozi.

" umechanganyikiwa au? kinachokufanya ucheke nini?" Malimbe anamuuliza na baada ya watu kuona kaacha kucheka Kila mtu anarudi na kuendelea na mazungumzo Yao lakini hiyo ni baada ya kumjadili Tulya kidogo.

" inafurahisha" anaongea Tulya akiwa bado anacheka kidogo.

"nini?" Lindiwe anauliza.

" Sasa hivi Haina umuhimu tena" anaongea Tulya akimwangalia Muli moyoni akijuta imekuwaje habari hii imemfikia kwa kuchelewa majibu ambayo angempatia mwanamke huyu kipindi anamnanga mume wake angekuwa anajua habari hii angeacha kula nyama maisha yake yote na kula majani kama mbuzi.Kukosa nafasi ya majibizano mazuri na mwanamke huyu vita ambayo angeishinda pasipo kutoka jasho ndicho kilichomfanya acheke.

" usije ukarudia tena kumnanga mume wangu kama unajipenda" anawaza Tulya moyoni akimwangalia Muli.

" mbona wanachelewa sana" anauliza akili ikirudi kwa mume wake macho yake yakiangalia njia anayohisi watatokea.

" watafika" anajibu Lindiwe anayeonekana Hana furaha na ujio wa mume wake.Tulya analiona hilo anaamua kupotezea.Kama yeye hataki mumewe arudi asitake na wetu wahamie porini anawaza.

" kulikoni wewe na ndugu yako?" anamsikia Malimbe akimnong'oneza na anajua anamzungumzia nani." ni hadithi ndegu" anaongea kifupi na muda huo wanasikia makelele ya sauti za kiume.

" Wamefika" anaongea Tausi ambaye tangu afike hapa hajatia neno.Sura yake ikinyooka kwa furaha akianza kupiga hatua kuelekea sehemu zinakotokea sauti.

Mapigo ya moyo wa Tulya yanaenda mbio baada ya kuona wanaume waliobeba nyama za wanyama mbalimbali zilizowekwa kwenye miti na kusaidiana kubeba wawili wawili begani.Macho yake yanaangaza huku na kule lakini hamuoni anayemtafuta.

Wanawake wanapiga vigelegele na kuwapatia maji na wawindaji wenye watoto walitoka lindo ndio waliokuwa na furaha zaidi baada ya kuwaona ndugu zao kwa mda mrefu.

Anaendelea kutafuta katikati ya mkusanyiko wa watu lakini bado hamuoni Nzagamba wala kaka zake.Macho yake yana tua kwa Tinde bwana harusi mtarajiwa na kumuona kabadilika kidogo tofauti na alipomuona mara ya kwanza mtoni akiongea na Sinde.Akiwa amesimama na Mama yake pamoja na dada yake.Anatabasamu moyoni akiwaza kwenda kumtania Sinde kuwa mume wake ana ndevu kama kalungu yeye.

" usihangaike wale wanamaliziaga Kila siku"

anamsikia Ntali akiongea baada ya kutaka kupiga hatua kwenda mbele zaidi kumtafuta mumewe maana imeshakuwa fujo hata haoni vizuri.

" kwa nini?" anauliza akijua labda ni sheria lakini Ntali anamthibitishia tofauti.

" madaha Yao tu" anamjibu.Tulya anakasirika moyoni kwani hawajui kama Kuna watu wana wasubiri au anajiuliza.

Wawindaji waliokwisha kufika wengi wao wakiwa ni vijana waliotoka lindo wanakaa chini kwa makundi na wanawake wanashirikiana kuwanawisha mikono na kuwapatia chakula kilicholetwa na Kila mtu wakichanganya na kuwa gawia.Tulya anaendelea kufanya kazi ya kutenga chakula Ili Hali akili yake ikiwa haipo pale.Labda mumewe atakuwa ameumia na tangu wamefika hajamsikia mtu yeyote akimzungumzia.

"mume wangu yupo sawa?" anamuuliza Tinde baada ya kujifanya kumpelekea chakula.Tinde anamwangalia kama kumuuliza ye nani kwani alimuona Tulya mara Moja tu na hamjui mume wake ni nani.

" Nzagamba" Tulya anamtajia jina na Tinde anamkumbuka kwani habari alipata kuwa Nzagamba amemuoa binamu yake Sinde mkewe mtarajiwa.

" sijui kwa sababu tulikuwa kundi tofauti lakini...." kabla hajamalizia anasikia sauti za watu wengine wakifika anaweka sahani chini na kuondoka haraka kuelekea zinapotokea sauti na sio yeye tu anamuona Tausi,Lindiwe,wifi zake na wanawake wengine wakielekea kule na vibuyu vya maji anapata uhakika kuwa waliofika ni wenyewe.kiungo chake kilichojificha katikati ya mbavu kinazidi kuongeza mdundo wake kikitishia kupasua ngome ya ulinzi wake.