webnovel

CHAPTER 8

Leah aliangalia saa ya ukutani tena kwa mara nyingine; saa saba kasoro usiku. Simu yake ilikuwa tupu bila meseji yoyote ya taarifa kutoka kwa mume wake. Uvumilivu ulikuwa umemshinda rasmi. Wiki zote zilizopita alijitahidi kuwa muelewa lakini hakuona mabadiliko yoyote. Nyumba ilibadilika sana. Hakukuwa na amani tena.

Akiwa sebuleni alisikia sauti ya gari la mume wake likiwasili. Leah alikaa mkao wa maongezi. Paul aliingia ndani. Tai yake ilikuwa imelegea na mikono ya shati ilikuwa imekunjwa. Alikuwa na uchovu lakini kwa bahati nzuri au mbaya, Leah hakutaka alale bila kuwasilisha changamoto mezani.

Leah alimkata jicho la hasira Paul, "Hivi unajua sasa hivi ni saa ngapi?", aliuliza, mikono ikiwa imekunjwa kifuani.

"Najua.", Paul alijibu kwa sauti kavu na ya kutojali.

"Embu nisaidie maelezo; Nini kinaendelea? Kama una malalamiko yoyote ni bora uyaseme. Tunatakiwa kuzungumza.",

"Usiku sasa. Tutaongea kesho.",

"Siwezi kusubiri. Tuongee sasa hivi.",

Paul alirusha begi lake kwenye kochi kwa kero, "Mimi na wewe, sioni matumaini tena.", alitamka,

"Ukimaanisha?", 

"Ndoa yetu imefikia kikomo.", 

Leah alipiga hatua chache kumkaribia, "Ni kitu gani kimepelekea wewe kufikia hilo hitimisho?",

"Sioni maana tena.",

"Kwasababu siwezi kubeba mimba?",

"Sababu ni nyingi, Leah. Usinifanye nizitamke moja baada ya nyingine.",

"Actually, ninataka kujua hizo sababu zote.", Leah alipaniki, "Kosa langu ni nini? Utofauti wako umeanza siku moja baada ya mimi kukwambia kuhusu matatizo ya kizazi changu. Unaniadhibu au?",

"Tatizo sio kwamba huwezi kubeba mimba. Kuna njia nyingine za kupata mtoto ambazo wewe hutaki kusikia. Hilo ndo tatizo.",

"Kingine?",

Paul aliangua kicheko cha kejeli na kilimshitua Leah. Alihisi ameongea jambo la kijinga.

"Unacheka nini?", Leah aliuliza.

"Dharau zako zinafurahisha sana. Hivi nikiwa naongea unakuwaga unanisikiliza? Tatizo una dharau sana Leah. Sijui ndo haujali hisia za wengine? Nimeshindwa.", 

"Dharau gani, Paul? Mbona miaka yote tumeishi vizuri tu na haujawahi kusema kitu kama hichi? Kama uliniona nina dharau ungeniambia tokea siku nyingi ili nijirekebishe.",

"Ishu ni kwamba huwezi kubadilika. Umeonesha kabisa kuwa upo radhi uwe peke yako kuliko kubadilisha uamuzi wako.",

"Paul.", 

Haikuwa rahisi kwa Paul kusema aliyoyapanga lakini hakuwa na jinsi, "Leah, kila lenye mwanzo lina mwisho.", Paul alisema, "Ndoa Yetu imefikia tamati. Upendo umeisha kabisa.",

"Kuwa makini na unachokisema, Paul.", mapigo ya moyo yalimwenda mbio. Alikwishajua muelekeo wa maongezi yale. Aliogopa. Ilimtisha.

Paul alifungua begi lake na kutoa bahasha kubwa. Aliiweka bahasha ile mezani.

"Leah, tuachane.", hatimaye alitamka.

"What?",

"Kwenye hiyo bahasha kuna fomu mbili za talaka zinazohitaji sahihi yako. Mimi nimeshaweka sahihi yangu. Tunakusubiri wewe.",

Leah alibubujikwa machozi bila kujua. Ilikuwa ghafla sana. Katika vitu ambavyo hakuwahi kutegemea ni ndoa yake kuvunjika. Leah alimpenda sana mume wake, na hakuwa tayari kumpoteza. Lakini kwa kuangalia tu aliona kuwa Paul tayari alikuwa ameshamkatia tamaa yeye na kila kitu walichojenga pamoja ndani ya miaka yao kumi ya ndoa. 

"Paul, embu punguza hasira na unisikilize mume wangu.", Leah alitamka kwa upole, "Najua nina mapungufu mengi. Hata wewe pia unayo. Lakini kuachana sio suluhisho. Ni bora tuambiane ili tubadilike.",

"Tumeshachelewa kubadilika. Maji yameshamwagika.", Paul aliongea bila tone la huruma.

Machozi ya Leah hayakumteteresha. Uamuzi wake ulikuwa umeshafanyika na hakutaka kurudi nyuma.

"Nitalala chumba cha wageni mpaka pale tutakapokamilisha talaka. Hata mimi inaniuma lakini hatuna budi kukubaliana na uhalisia.", alisema Paul kisha kuchukua begi lake na kuondoka sebuleni kuelekea kwenye chumba cha wageni.

Leah alipigwa na bumbuwazi. Alidondoka kitako kwenye kapeti lakini hata maumivu hakuyasikia. Mwili mzima uliingiwa ganzi. Jibu alilokuwa akilisaka siku zote hatimaye alilipata, lakini jibu hilo lilikuja kama mkuki wa moyo. 

Miaka kumi ya ndoa, milima na mabonde, eti ndio vimeishia hapo? Bila sababu ya muhimu? Akili iliyumba. Alibaki macho wazi akitazama patupu. Machozi yaliendelea kutiririka na hakuweza hata kunyanyua mkono kuyapangusa.

"Naomba niwe mkweli.", aliongea mtangazaji yule.

Asubuhi na mapema redio zote zilikuwa wazi na kipindi chake kilikuwa hewani. Wiki ya nne, wiki ya mwisho kama alivyoahidi. Siri za watatu tayari alikwishazifichua. Sasa alibaki mmoja tu; Leah.

"Katika watu niliohangaika sana kupata taarifa zao ilikuwa ni Leah. Jamani eeh, dada yetu haishi maisha mazuri. Hizo picha na video anazoposti zote ni uongo. Hivi mtu unakaaje kwenye ndoa miaka 10 bila kupendwa? Yani unakuwa unatafuta nini haswa?", alisema mtangazaji yule, "Nina swali kwa dada yetu Leah. Hivi unafahamu sababu ya mume wako kutaka kuwa mwanasheria? Unajua ni sehemu gani huwa anakwenda kila Alhamisi na Ijumaa? Unajua kwanini mume wako ameamua kukupa talaka? Jibu ni hili hapa; Mume wako hakupendi na hajawahi kukupenda.",

Mtangazaji alimwaga mchele kwenye kuku wengi.

"Kabla mume wako hajakutana na wewe, alikuwa kwenye mahusiano na mwanadada mmoja hivi. Walisoma wote kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tano. Kabla hawajaingia kidato cha sita, dada yule alikumbwa na kesi ya kumuua baba yake wa kambo. Hatujui kama ni kwa bahati mbaya au alikusudia. Kwa kuwa mume wako alimpenda sana yule dada na bado anampenda, alipomaliza kidato cha sita alienda chuo kusomea sheria. Nia na dhumuni siku moja aje kumtoa mpenzi wake gerezani. Baada ya familia ya baba wa kambo kugundua nia yake, wakakataza kabisa Paul na huyu dada kuonana hivyo ikawa ngumu kwa Paul kufungua tena hii kesi. Na kipindi hicho akiwa na stress na upweke mkubwa ndipo akakutana na Leah.", mtangazaji alieleza, "Mapenzi kwa girlfriend wake hayakuisha. Kila Alhamisi na Ijumaa kwa miaka nane mfululizo, Paul hajawahi kukosa kumtembelea dada huyu. Kwa habari za uhakika nilizozipata, dada huyu kifungo chake kinaisha baada ya wiki tatu na atakuwa huru. Ndiyo maana Paul ameamua kumuacha Leah solemba. Maskini.",

***