webnovel

CHAPTER 4

Katika sehemu ambazo Suzanne hakupenda kwenda ilikuwa ni hospitali ya St. Monica, iliyohusiana na kutibu watu wenye magonjwa ya akili. Suzanne hakupenda muonekano wa jengo, harufu na watu wote aliokutana nao humo ndani. Ilikuwa ni mgonjwa mmoja tu ambaye alimfanya Suzanne apige moyo konde na kwenda hospitali hapo. Mgonjwa huyo alikuwa ni Flaviana.

Suzanne alikuwa kwenye chumba maalumu cha matembezi akisubiri manesi wamlete Flaviana. Kadili ya sheria za hospitali hapo, simu yake ilikuwa mbali na yeye. Hivyo hakuweza kusikia meseji na simu zilizokuwa zikiingia kama mvua.

Hatimaye Flaviana aliwasili kwenye chumba kile. Alikuwa ni mdada mweusi, mrefu mwenye sura nzuri ila iliyochoka. Alivaa gauni ya wagonjwa ya rangi ya kijani na nywele zake zilikuwa kwenye mtindo wa twende kilioni. Midomo yake ilikuwa imekauka na alikuwa na michubuko michache kwenye miguu yake. 

Nesi alivuta kiti nyuma na kumkalisha Flaviana kitako, kisha nesi yule aliwaachia nafasi na kutoka nje. Sekunde zilizofata zilijaa ukimya, Suzanne na Flaviana wakitazamana kwa macho ya hasira.

"Umekuja kufanya nini?", aliuliza Flaviana,

"Unajua kilichonileta, usiniletee ujinga. Michoro ipo wapi?", Suzanne aliuliza kwa hasira ya chini.

"Michoro gani? Sijui unaongelea nini?",

"Sikiliza Flaviana; ukijifanya mjuaji utazeekea humuhumu. Hautapata nafasi ya kuiona dunia nje ya mageti ya hii hospitali.",

"Sidhani kama kuna utofauti mkubwa. Bora humu ndani nina marafiki.", alisema Flaviana.

Suzanne alisogeza kiti chake mbele, "Nina uwezo wa kubadilisha maisha yako kuwa mazuri au mabaya zaidi.",

"Maisha yangu yalikuwa mazuri, Suzy. Nimesoma, nina vyeti, nina akili timamu na nina kipaji kikubwa. Wewe hauna kitu chochote! Vyote ulivyonavyo ni vyangu!", Flaviana aliongea kwa mkazo, machozi yakimlengalenga.

"Are you stupid?", Suzanne alifoka.

"Kama kweli unakipaji kama unavodanganya watu, kwanini umetuma watu wawe wanaiba michoro yangu na kukuletea wewe? Nguo zote unazojifanya umedesign wewe zimetoka kwenye kichwa changu.",

Suzanne alimchapa Flaviana kibao cha shavu lakini aliingiwa na woga wa ghafla pale alipoona Flaviana akitabasamu badala ya kulia. 

"Ulihisi sijui kinachoendelea? Umefeli Suzy. Kwa taarifa yako, dunia nzima imeshajua ukweli. Angalia simu yako.",

Kwa haraka, Suzanne alifungua mkoba wake na kutoa simu yake. Alishangaa kukuta simu na meseji tele. Vidole vikitetemeka, alifungua meseji ya juu kabisa. Meseji hiyo ilisema;

Suzy, habari zako zimewekwa wazi. Ni kweli uliiba idea ya kampuni yako kutoka kwa binamu yako?

Mapigo ya moyo yalianza kumuenda mbio. Alinyanyuka akihema na kutoka nje ya chumba kile kwa haraka. Flaviana alicheka kwa nguvu, "MALIPO NI HAPA HAPA!", alisema kwa sauti.

Suzanne alikuta sekretari wake akimsubiri nje ya gari akitweta.

"Madam, nilikuwa najaribu kukupigia _",

Suzanne alimpuuzia sekretari wake na kupanda kwenye gari. Akiwa ndani aliwasha redio.

"Suzanne na Flaviana walikua pamoja kama ndugu wa damu moja. Baada ya wazazi wa Flaviana kufariki kwenye ajali, baba yake Suzy alimchukua Flaviana na kumlea kama mwanae. Shida ilitokea baada ya Flaviana kuonesha uwezo mkubwa wa kiakili akiwa shuleni huku Suzy akiwa kilaza.", alisema mtangazaji yule asiyejulikana.

Suzy alikuwa akitetemeka ingawa jua lilikuwa kali nje.

"Nilichowapendea wazazi wale ni kwamba waliwekeza pesa zao kwa mwenye uwezo. Hivi mnafahamu kuwa Flaviana ana degree ya fashion designing and marketing kutoka France? Kipindi hichohicho, Suzy alikuwa akisomea diploma ya hotel management and tourism nchini Mauritius. Future ya mwenzie ilikuwa inang'aa na hilo lilimtia sana wivu Suzy, hivyo akafanya mpango wa kuharibu maisha ya mwenzie.",

Simu ya Suzy ilianza kuita tena. Kwa hasira alifungua mlango na kuirusha nje. Sekretari wake alikimbia kwenda kuiokota.

"Flaviana alipomaliza chuo alirudi nyumbani na degree yake na idea yake ya biashara, ambayo ni hii kampuni iliyo chini ya Suzy tunavyoongea. Kwakuwa Flaviana alimpenda sana Suzy na kumuamini, alimwambia yeye wa kwanza. Lakini katika zile story, Suzy alitegesha dawa kwenye kinywaji cha mwenzie. Usiku mzima, kichwa kilimuuma sana Flaviana. Asubuhi ilivyofika, macho yalikuwa hayaoni na maneno aliyokuwa akitamka yalikuwa hayaeleweki.",

Jasho jembamba lilimtoka Suzy akisikiliza. 

"Wazazi walichanganyikiwa. Muda huohuo, Suzy tayari amekwisha iba idea ya mwenzie ya kampuni na mitindo yote aliyokuwa ameichora. Hata hospitali ilivyopatikana, Suzy alikula dili na manesi wawe wanamzidishia dozi ndugu yake ili akili zizidi kupotea. Flaviana wa watu masikini akawa kama kichaa. Lakini Mungu si Athumani, bado kipaji chake alibaki nacho na alikuwa akichorachora. Manesi wa hospitali ya St. Monica wakawa wanachukua michoro ile na kumletea Suzy kisha Suzy akawa anadanganya watu kuwa amechora yeye. Inasikitisha sana.",

Suzy alizima redio na kupiga kelele za hasira. Shati aliyokuwa amevaa ililowa jasho. Sekretari wake aliingia ndani ya gari.

"Unataka nifanye nini, madam?", aliuliza Hope.

"Take me to the radio station right now!", Suzanne alifoka.

Hope alitii.

FARAJA STATION

Getini kulikuwa na walinzi watatu, wote wakizuia gari la Suzanne kuingia ndani. Maagizo yalikwisha kutolewa kuwa Suzanne haruhusiwi kuonekana eneo lolote karibia na stesheni ile. Kichwa kilimgonga sana kutokana na kelele za walinzi wale wakikwaruzana na sekretari wake.

"Hatujaja hapa kufanya vurugu.", alisema Hope, "Tunataka kuongea na mkurugenzi.",

"Samahani ila onyo limetolewa tayari. Hatuwezi kuwaruhusu kuingia.", alisema mlinzi.

Simu ya Suzanne iliita ghafla. Jina 'BABA' lilisomeka kwenye kioo. Mikono ilianza kumtetemeka tena na moyo ulimwenda mbio. Aliweza kufikiria maneno yote ambayo baba yake alikuwa ameshapanga kumwambia, na ilimuogopesha sana. Matokeo yake alishindwa kupokea simu ile. Aliiacha iite.

"Hope, tuondoke.", alisema Suzanne kwa sauti ya chini.

Hope alifunga kioo na kuondoa gari. 

Njia nzima Suzanne alijaribu kupigia watu wake wote wa karibu lakini hakuna hata mmoja aliyepokea simu yake. Machozi yalimtoka bila yeye kujua. Kila dakika ilikuwa mbaya kuliko nyingine. Hatimaye alipata wazo la kumpigia Janat. Simu iliita kwa sekunde chache kisha kupokelewa. Suzanne alivuta pumzi ya auheni.

"Janat, afadhali umepokea. Unaweza ukaongea na wengine ili tuweze kukutana?", aliuliza Suzanne.

Janat aliguna, "Mh, Suzy, haitawezekana.", aliongea.

"Kwa-kwanini? Why?",

"Habari zako tayari zimeshasambaa nchi nzima. Haitakaa vizuri kwetu kama tukionwa tupo na wewe.", Janat alieleza bila kusita.

"Unamaanisha nini, Janat? We're friends.",

"Najua, ila si unajua usemi unavoenda; samaki mmoja akioza.",

Suzanne hakuamini masikio yake. Kati ya wote watatu, yeye alikuwa na ukaribu mkubwa sana na Janat. Walishibana. Haikuwahi kutokea siku waliyokorofishana. Kama kugeukwa, Suzy alitegemea usaliti huo utoke kwa mtu mwingine na si Janat.

"I can't believe this.", alisema Suzanne kwa sauti iliyojaa mshangao.

"Sorry Suzy. Tunaprotect our image.", Janat alijitetea.

Suzy alitoa kicheko cha uchungu, "Sikia Janat; yule mtangazaji alisema ana habari kuhusu sisi wote wanne. So, if you think mimi peke yangu ndo nitayemalizika, kaa ukijua your turn is coming.",

"Ulikuwa unafikiria nini kumpa madawa cousin wako?",

"Usiniulize maswali!", Suzanne alifoka, "I really hope you're next. I hope she cuts your wings and crushes you to the ground.",

Kwa hasira Suzy alikata simu.

***

Next chapter