4 CHAPTER 3

Jioni ilipowasili ilikuwa ni Suzanne, Janat na Annabella tu waliokuwa wameketi kwenye meza ya chai. Kwasababu ya faragha, chumba walichokuwa wakinywea chai kilikuwa mbali na macho ya watu. Waliomba usiri mkubwa.

"Tumsubiri au tuendelee?", aliuliza Annabella.

"Ndio kwanza saa kumi na moja na dakika kumi. Labda yupo njiani.", alijibu Janat.

"Umeongea na secretary wake?", aliuliza Suzy.

"Mara ya mwisho kuongea nae ni leo asubuhi. Aliongea na secretary wangu.", Janat alijibu.

"Anaweza asije. Kama alishindwa kuja pale station kuleta malalamiko, sisi ni nani?", Suzy bado aliendelea kubisha.

"Hivi ni mimi peke yangu ndio naona kuwa Leah haoneshi uoga wowote kuhusu hili swala?", Annabella aliuliza.

"Hakuna _",

"Kwanini nioneshe uoga?", alisikika Leah akiongea, kumkatisha Janat.

Vichwa vyao viligeukia mlangoni. Leah alikuwa amewasili. Alijongea mezani na kukaa kwenye kiti kilichoandaliwa kwa ajili yake. 

"Nimeitikia wito.", alisema Leah.

"Mwenzetu, mbona hili swala linaonekana kutokukusumbua?", Annabella aliuliza tena.

"Cha kwanza; njia yangu ya mafanikio ni safi. Sijawahi kuzurumu, kuua au kuumiza mtu yoyote. Nimepambana mimi na nafsi yangu mpaka hapa nilipofikia.", Leah alijibu.

"Kwahiyo unasema sisi tunaopanick tumeua watu au?", Suzy aliuliza.

"Sijasema hivyo. Nilichomaanisha ni kwamba, kama mnajiamini na amna kitu kibaya mlichofanya, hakuna haja ya kupanick na kuitana vikao vya maficho kama hivi.",

Suzanne alimpandisha Leah juu mpaka chini na kusonya. 

"Binadamu wapo hivi; kuliko waamini ukweli, wapo radhi kuamini uongo hata kama haueleweki. Yule mtangazaji wa Faraja amejipanga kusema mambo mabaya kuhusu sisi.", alisema Janat.

"Na matokeo yake ni kuwa kila kitu tulichotolea jasho kinaenda kuharibika; biashara zetu, familia zetu na mahusiano yetu. Kila kitu. ", Annabella aliongezea.

"Tena wewe Leah unaesema kuwa njia yako ya mafanikio ni safi ndo unatakiwa kuogopa zaidi.", alisema Suzanne.

"Kwanini?", Leah aliuliza.

"Kwasababu vitu vibaya atakavosema kuhusu wewe vitakuwa ni uongo mtupu. Hivi upo tayari kupoteza mafanikio yako kwa sababu za uongo? Tena zilizotungwa na mtu hata usiyemfahamu? Haikutishi?", Suzanne aliuliza kwa kituo na mkazo.

Leah aliweka kikombe cha chai chini na kuegamia kiti. Alikunja mikono yake kifuani, "Sasa lengo la hichi kikao ni nini?", aliuliza.

"Tusaidiane kumjua huyu mtangazaji ni nani na tuweze kukutana naye kabla hajatoa hivyo vipindi vyake.", alisema Janat.

"Nasikia mlienda kumuona Rajabu. Yeye hakuwaambia?", Leah aliuliza,

"Rajabu aligoma. Ameamua kumficha.", alisema Annabella.

"Lakini tukishirikiana, tunaweza kumfichua.", Suzanne alisema.

"Okay. Mimi naona kila mtu atumie njia zake za kupata taarifa za huyo mtangazaji. Kila hatua tutayofikia tutakuwa tunajulishana.", Janat alichangia na wazo lake lilipitishwa na kila mtu. Walikubaliana kushirikiana ili kuzuia majanga yasiwakute.

Siku haikuwa nzuri kwa Paul. Japo kuwa mke wake alimuomba msamaha asubuhi, bado alikuwa na dukuduku rohoni. Paul alikuwa karibu sana na mama yake mzazi. Vitu vingi alivyoshindwa kujadiliana na Leah, alikwenda kuviongea na mama yake. Jioni ile baada ya kumaliza kazi, Paul aliendesha gari mpaka nyumbani kwa mama yake. Alipowasili, alikuta tayari ameshatengewa chakula mezani kwani alitoa taarifa ya ujio wake mapema. 

Ingawa mama yake umri ulikuwa umeenda, alijipenda sana. Alikuwa mwanamke maridadi na mwenye kupenda vitu vya gharama. Hata nyumba yake, fenicha na vyombo vya ndani vilikuwa vya bei ghali. 

"Nina mawazo mama. Nisipoongea na mtu nahisi kichwa kinaweza kupasuka.", Paul alianza kuzungumza,

"Mawazo gani?", mama aliuliza,

Kwa sekunde chache, Paul aliweka uso wake ndani ya viganja vyake vya mkono. Jambo hilo lilimpa hofu kubwa sana mama yake. Miaka mingi ilipita tangu amuone mwanae akiwa kwenye mawazo makali namna ile. Hakufurahishwa na ile hali.

"Nini kinaendelea? Kazini kupo salama?", mama aliuliza kwa wasiwasi.

"Kazini kupo salama. Ni nyumbani. Maji yamenifika shingoni. Sijui nifanyeje?", Paul alieleza.

"Umegombana na mke wako?",

"Tulikwaruzana kidogo jana usiku ila leo asubuhi aliniomba msamaha. Lakini mama, hii sio mara ya kwanza. Leah huwa ananivunjia heshima kila akipata nafasi, alafu anaomba msamaha. Inaniumiza mama, kwasababu maneno anayokuwa amenitamkia yanabaki kichwani.",

"Embu nielezee vizuri. Sababu ya nyie kukwaruzana jana ilikuwa ni nini?",

Paul alimtizama mama yake. Hakujua kama ni jambo sahihi kumwambia kisa kizima maana itamgarimu kusema kuusu swala la uzazi la mke wake. Wakati huohuo, Paul hakuweza kumficha mama yake kitu. Alimuamini asilimia mia moja.

"Leah alienda kumuona daktari jana. Kwa bahati mbaya amekutwa na tatizo kwenye kizazi. Hana uwezo wa kushika mimba.", Paul alielezea.

"Nini?", kwa mshituko mkubwa, mama aliachia kijiko, "Leah hawezi kuzaa?",

"Ndio.",

"Kwa maana nyingine siwezi kupata mjukuu?",

"Ndio mama.",

"Haiwezekani.",

Mama alinyanyuka kwa hasira na kuondoka kwenye chumba cha chakula. Paul alimfata mama yake. Koo lilimuwasha kutokana na maneno mengi aliyopanga kuyaongea.

"Mama.", aliita.

Mama yake alisimama na kumgeukia. Mikunjo ya hasira ilionekana kwenye paji lake la uso.

"Huoni kama hii ni bahati mbaya kwenye familia yetu?", aliuliza mama, "Familia yetu inahitaji kukua. Nahitaji wajukuu. Wewe ni mtoto wangu pekee. Siwezi kulichukulia hili jambo kirahisi.", aliendelea kulalamika.

"Leah hakupenda kuwa na hilo tatizo _",

"Mimi simuongelei Leah, nakuongelea wewe. Wewe unaona ni sawa mkae tu bila mtoto? Kwasababu gani? Huitaji damu yako? Uwezo wa kupata mtoto, au watoto unao. Kwanini unajiwekea kikomo?",

"Mama, Leah ni mke wangu. Siwezi nikamfanyia hivyo.", Paul alijitetea.

"Sikiliza; umeshasema hakueshimu. Nakumbuka nimeshawahi kukwambia kuwa Leah anakudharau kwasababu ya pesa zake. Atakuja kukuvua nguo mbele za watu. Hilo moja. Mbili; hana uwezo wa kukupatia watoto. Tatu; umesikia tetesi zinazoendelea? Sijui huyu mtangazaji amegundua nini kuhusu Leah na matajiri wenzie, lakini halitomuangusha Leah tu. Wewe pia utawekewa doa. Familia yetu nzima itawekewa doa.", alisema mama.

"Unazidi kunichanganya.", Paul alikuna kichwa.

Mama alimsogelea mwanae na kumshika bega, "Si umekuja kuomba ushauri? Sasa ushauri wangu ni huu; majanga haya yote yanaweza kuepukika, na njia ya kuyaepuka unaijua.",

Paul alielewa fika nini mama yake alikuwa akimaanisha. Ni wazo ambalo hata yeye alikuwa nalo kichwani ila aliogopa kuliendekeza. Kitendo cha mama yake kugusia hapohapo ambapo alikuwa anapafikiria mara mbili kilimpa matumaini na nafuu ya roho. Labda lilikuwa ni jambo sahihi. Labda.

...

"Wahenga walisema ahadi ni deni.", ilisikika sauti kutoka redioni, "Kama nilivowaahidi wananchi wa Tanzania, leo natoa taarifa kamili kuhusu dada yetu tunayempenda; Suzanne Depo.",

***

avataravatar
Next chapter