20 CHAPTER 19

Usiku uliingia. Reuben alimaliza kikombe cha pili cha kahawa. Bado alikuwa kituoni akijaribu kutatua kesi mbili zilizofungamana; kesi ya mauaji ya Montana na mama Zai, na kesi ya ajali ya Cecy. Joy alirudi kutoka msalani na matumaini ya kupumzika yalipotea baada ya kumkuta Reuben akitengeneza kikombe cha tatu cha kahawa.

"Hakuna kulala leo?", Joy alitania,

"Nahisi nakaribia kuimaliza hii kesi lakini kuna kitu kimoja nashindwa kukielewa. Nikiweza tu kukifahamu hicho kitu, kesi imeisha.", alisema Reuben na kunywa kahawa yake,

"Detective, uliamini maelezo ya Leah?",

"Yeah.",

"Sasa inamaanisha umeamini maneno ya wote wanne. Mmoja kati yao ni muongo na muuaji.",

"Joy, what if wote wanne hawana hatia?",

"Lakini mama Zai alisema _",

"What if mama Zai alikuwa blackmailed?",

"By who?",

"Muhusika mkuu.",

"Ambaye ni nani?",

Reuben aliangalia kahawa yake na kutabasamu, "A man.",

Leah alitoka bafuni huku akijipangusa maji. Simu yake iliyokuwa kitandani ilianza kuita na mpigaji hakuwa mwingine bali Babra. Kwanza Leah hakutaka kupokea, lakini kuna kitu, sauti, ilimfanya apokee asikie ni nini Babra alitaka kusema;

"Babra _",

"Boss, nisikilize. Sikutaka kufanya hili jambo, sikutaka kukusaliti. Wewe ulikuwa mtu mwema sana kwangu. Sikutaka nikuumize.",

"Umeshaniumiza, Babra.",

"Alinifosi na kutishia kumuua mama yangu. Alitulazimisha wote wanne. Alituahidi kuwa tukiweza kupata siri kubwa za mabosi zetu atatupa kila mtu milioni 50. Wengine wote waliweza kupata hizo siri lakini mimi sikuweza kwasababu haukuwa na siri yoyote kubwa. Ilibidi niweke recorder ili nipate chochote tu cha kumwambia Montana.",

Uso wa Leah ulikunjika kwa maswali yaliovamia ubongo wake, "Mlilipwa pesa za kutuchafua?", aliuliza,

"Ndio. Mimi, Ariana, Hope na Thomas, kila mmoja alipewa kazi za kutafuta siri za bosi wake. Hatukujua kuwa angetugeuka. Kifo cha Montana hakikupangwa. Alimuua ili kutuonya tukae kimya.",

Kwa mbali Leah alisikia mlango wake wa sebuleni ukifunguliwa. Haraka alivaa gauni lake la kulalia.

"Bosi, ulipokuwa kwenye kikao, mimi ndio nilichukua simu yako na kumtumia message Cecy. Uliharibu mipango yake yote ulipoenda kukutana na Cecy gerezani, hivyo akaona amuue na akupakazie wewe kesi.",

"Babra.", Leah alinong'ona, "Nani alikufosi?",

"I'm sorry boss. He's coming.",

Mlango wa chumba ulipigwa teke na Paul aliingia. Kwa mshituko mkubwa Leah aliangusha simu. Paul alikuwa kama faru litwetalo kwa hasira. Alianza kumsogelea Leah kama mwindaji;

"Umeyataka yote haya.", Paul alianza kuzungumza,

Leah aliangalia huku na huku akitafuta pa kukimbilia.

"Nilijua tu nikikwambia tuachane utakataa. Ubishi wako umekuponza.",

"Paul, please, just simama tuongee.", Leah aliogopa sana,

"Leah, Leah, Leah, mke wangu Leah. Kwanini uliamua kutajirika na kuanza kunidharau?",

"Sijakudharau, tafadhali.",

Leah alikimbilia bafuni lakini kabla hajafunga mlango Paul alishika kitasa na kuusukuma. Leah alinguka na kutegua mkono wake. Sasa hakuwa na pa kukimbilia. Paul aliinama chini na kukamata shingo ya Leah kwa nguvu. Alianza kumkaba.

Leah alijaribu kurusha mikono na kumsukuma lakini alimzidi nguvu.

"Ulijiona upo perfect, sio?", Paul aliendelea, "Ukaona umenizidi akili, sio? Ukaenda kumshawishi Cecy awe upande wako. Mpumbavu mkubwa wewe. Nyie wote wapumbavu!",

Leah alianza kukosa pumzi. Alitapatapa bila mafanikio.

"Ukifa mali zako zote zitakuwa zangu. Bora ungekubali talaka. Na wapumbavu wenzio wote nimewaangusha; Janat anaenda jela kwa miaka mingi sana, wengine hawataionja dunia ya kitajiri tena, na wewe leo utaiaga dunia.",

Viini vya macho vilianza kupanda juu huku rangi ya uso wake ikibadilika. Aliyaona maisha yake yote yakipita mbele ya macho yake. Hapo alipata jibu alilokuwa akilitafuta siku zote. Ni wapi alikosea. 

2009; sherehe za chuo. Leah hakutaka kwenda, lakini marafiki zake walimlazimisha. Huko alikutana na Paul, kijana mtanashati na mwenye aibu. Wawili waliona ni vyema watoroke waende sehemu ya peke yao yenye ukimya. Walianza kuulizana majina, kisha miaka, kisha kozi walizokuwa wakisoma hapo chuo. Stori za hapa na pale na Paul alifanikiwa kumchekesha Leah. Walibadilishana namba za simu na moyo wa Leah ulimkaribisha Paul bila itirafu. 

Mwaka 2010 walisimama kanisani mbele ya familia zao na Mungu na kuapa kupendana na kuvumiliana kwenye shida na raha, hadi kifo kitakapowatenganisha. Nao wakafanywa mwili mmoja, familia moja.

Labda asingeenda kwenye ile sherehe mwaka 2009, maisha yake yasingekuwa yakikatishwa. Kijana yule mzuri, aliyevaa miwani kubwa na mwenye aibu leo hii alikuwa kaweka mikono yake shingoni akikamua maisha yake yatoke. Mwaka 2009 ndio chanzo.

"KUFA! KUFA! KUFAAA!", Paul aliunguruma kama ana wazimu.

Leah aliona giza, kitu pekee masikio yake yakisikia kuwa ni ombi la mume wake kumtaka afe. 

"What a sad life.", Leah alijisemea kimoyomoyo, "Kumbe hichi ndo kifo changu? Can't believe I used to kiss his hands, unaware that one day the same hands will kill me.",

Hatimaye Leah aliacha kutapatapa;

"MIKONO JUU!", ilisikika sauti kutoka mlangoni.

Paul aliachilia shingo ya Leah na kugeuka nyuma. Hakutegemea kukutana na kundi la askari, Reuben na Joy. Maaskari wawili walimvuta Paul nyuma huku wengine wakimbeba Leah na kumuwahisha nje. Leah alikuwa kapoteza fahamu. Vyote vilivyoendelea hakusikia hata kimoja. 

Mikono ya Paul ilifungwa pingu. Wazimu wake ulizidi.

"Paul, upo chini ya ulinzi kwa kifo cha Montana, mama Zai na kosa la kukusudia kumuua Cecilia.", alisema Reuben,

Askari walimswaga Paul nje, kelele zake zikitawala nyumba. Joy alivuta pumzi. Kesi ilikuwa imekwisha rasmi.

"Detective.", Joy aliita, "Ulijuaje ni yeye?",

"Maelezo ya mama Zai.", alisema Reuben, "Aliposema kuwa ni mwanamke ndiye kamuua Montana, alikuwa anazifanya akili zetu zisiwaze upande mwingine. Pia unakumbuka Leah alichosema jana? 

"Kuhusu kuzungumzia talaka usiku alafu habari zikatangazwa asubuhi?",

"Yeah, inamaanisha mmoja wao alikuwa na access ya Montana. Mtu ambaye ni Paul. Jana jioni Leah alikuwa na kikao mpaka usiku na ushahidi upo. Huyu dereva aliyekuja kujiripoti alijichanganya. Naona Paul hakumpa maelezo yaliyonyooka.",

"And Paul amewezaje kupata taarifa zote za kina Suzy?",

Reuben alitoa simu yake na kumkabidhi Joy. Kulikuwa na ujumbe mrefu uliosema;

Paul alituahidi milioni 50 tukiweza kumpatia siri za mabosi wetu. Tulipofanikiwa na habari kusambaa alimuua Montana na mama mwenye nyumba ili kutuonya tukae kimya. Alisababisha ajali ya Cecilia ili amuue na kumpakazia kesi Leah. His last target ni Leah. Naomba mumuokoe.

 Babra.

"Wow! Asante Mungu tumewahi.", alisema Joy.

avataravatar
Next chapter