webnovel

CHAPTER 10

Kituo kikuu cha polisi Dar es salaam kilijiwa na ugeni wa Bwana Reuben Pasua.

Bwana Reuben alikuwa ni mpelelezi mkuu wa jeshi la polisi Tanzania. Alikuwa mbunifu na mwenye uwezo mkubwa wa akili. Macho yake yaliweza kuchuja uwongo, na pua yake iliweza kunusa uovu wa kila aina. Kwa miaka mitano Reuben hakuchukua kesi yoyote. Alitumia muda huo kutembelea nchi mbalimbali Asia, Ulaya na Amerika ya kaskazini ili apate kujifunza kutoka kwa wapelelezi wenzie waliomzidi uzoefu.

Kifo cha Montana Sabas kilikuwa kama mwaliko wa kumrudisha Reuben kazini. Usiku mzima alihisi maelezo ya polisi na hospitali hayakujitosheleza. Na siku zote kesi ikimnyima usingizi ujue kuna jambo lililojificha ambalo yeye pekee anaweza kulifichua.

Mkuu wa kituo cha polisi, Bwana Msumari, alimpokea Reuben kwa mikono miwili. Uwepo wake mahali hapo ulikuwa ni baraka. Lakini Bwana Reuben hakuwa peke yake. Alikwenda na msaidizi wake, mwanadada Joy Augustine, aliyehitimu chuo kikuu cha Dar es salaam mwezi mmoja uliopita. Joy alikuwa akifanya vizuri sana kwenye masomo, na ufaulu wake ulikuwa wa juu. Baada ya Reuben kusikia habari zake, alimpatia ofa ya kazi kabla ya sherehe yake ya kuhitimu. Sasa wawili wale walifanya kazi pamoja.

Siku zote Reuben alikuwa akimfundisha kwa mdomo. Sasa ulikuwa wakati wa vitendo. Wakiwa ofisini mule, bado Msumari alikuwa na amshaamsha ya kuwahudumia. Hakuamini kuwa ameketi uso kwa uso na Reuben.

"Bwana Reuben, ninafurahia uwepo wako, lakini najua kwamba una sababu kuu ya kufika hapa siku ya leo.", alisema Msumari.

"Bila shaka. Mkuu, ningependa kuona faili la Montana Sabas.", Reuben alisema.

"Sawa, ila ningependa kujua ni kwanini unaliomba.",

"Kuna jambo linanipa maswali. Pia ningependa kumuhoji mama mwenye nyumba. Mnasema yeye ndie aliyeukuta mwili wa marehemu, sio?",

"Ndiyo.",

"Nina maswali machache kwake.",

"Hakuna shida. Ofisi yangu nzima itakuonesha ushirikiano wa hali ya juu.",

Msumari alichomoa simu yake ya mezani na kumpigia aliyehusika na kutunza faili za kesi.

"Eh, niletee faili la Montana Sabas ofisini kwangu. Pia mpigie simu mama mwenye nyumba. Mwambie anahitajika hapa kituoni haraka iwezekanavyo.", Msumari alimuamrisha.

Ndani ya dakika kumi, faili lilikuwa mikononi mwa Reuben na simu kwa mama mwenye nyumba ilikwishakupigwa. Kwa umakini Reuben alilipitia faili lile kisha kumkabidhi Joy.

"Lisome alafu uniambie umegundua nini.", alisema Reuben.

Joy alifanya kama alivyoambiwa. Alipomaliza kulisoma, alikuwa na maswali elfu kichwani mwake. 

"Detective.", Joy alianza,

"Naam.", Reuben aliitikia,

"Hili faili linaonesha kuwa Montana alikuwa na maisha ya kawaida sana. Hata chumba alichokuwa amepanga hakikuwa cha bei kubwa. Mtiririko mzima wa maisha yake ulikuwa ni wa watu wa uchumi wa chini kidogo.",

"Kwahiyo?",

"Kutokana na kiwango chake cha maisha, sidhani kama ameweza kupata taarifa za ndani kabisa za matajiri hawa wanne bila msaada wa mtu mwingine.",

"Na ni mtu gani huyo aliyemsaidia Montana kupata habari hizo?",

"Bado nipo nafikiria. Lakini kwa harakaharaka, mtu huyo ana uwezo mkubwa wa kifedha na anawajua kiundani matajiri hawa wanne. Also, mtu huyo ana connections na watu wakubwa na ndio maana ilikuwa rahisi kuficha taarifa zote zilizohusiana na Montana.", alisema Joy.

Msumari aliwasikiliza kwa makini huku akijiuliza kwanini polisi wake hawakufikiria yote ambayo Joy na Reuben wanayazungumzia. Utendaji kazi wao ulimvutia.

"Let's nickname the mastermind as tajiri.", alisema Reuben, "So, tajiri alimfata Montana na ofa ya kufichua siri za wanawake hawa wanne. Kwa lugha nyingine alimtumia Montana kama mbuzi wa kafara. Maswali ya kujiuliza; Je, kwanini alimfata Montana na si mtu mwingine? Swali la pili; kwanini tajiri huyu aliingiwa na haja ya kufichua siri za wadada hawa? Dhumuni lake lilikuwa ni nini?",

Hodi ilibishwa mlangoni na kusitisha maongezi yaliokuwa yakiongelewa. Askari mwanaume aliingia ndani. Akiwa mlangoni, na kabla ya kufungua mdomo wake alipiga saluti.

"Mkuu, mama mwenye nyumba amewasili. Tumemuweka kwenye chumba cha maswali.", alisema askari yule.

"Vizuri. Msindikize Bwana Reuben na msaidizi wake. Wao ndio wana shida naye. Pia naomba muwaoneshe ushirikiano mkubwa.", alisema Msumari,

"Ndiyo mkuu.",

Reuben na Joy walinyanyuka na kumfwata askari yule.

Jasho lilijaa kwenye viganja vya mama Zai, mama mwenye nyumba. Hakuwahi kuhojiwa na polisi. Alihofia kuwa akikosea hata neno moja atakwenda jela. Alikosa amani. 

Mlango ulifunguliwa kisha Reuben na Joy waliingia ndani. Waliketi kwenye viti vyao vikimtazama bibie. Umri wa mama Zai na Reuben haukuwa mbali sana. Joy alikuwa mdogo kwao hivyo aliona ni vyema awaache wao waongee alafu yeye arekodi mazungumzo kupitia simu yake. 

"Umeshawahi kuhojiwa na polisi?", Reuben aliuliza,

"Hapana. Sijawahi.", mama Zai alijibu.

"Okay. Usiwe na wasiwasi. Nina maswali tu machache nayotaka kukuuliza. Nikishapata majibu yangu utakuwa huru kuondoka. Niambie ukipata njaa. Tunaweza pia kukupatia chakula. Maswali yangu yanaweza kuchukua muda kidogo.",

"Sa-sawa.", sauti ilimtetemeka, hakujiamini.

"Nitaanza na swali la kwanza. Montana aliishi kwako kwa muda gani?",

"Miezi mitano.",

"Katika hiyo miezi mitano, alikuwa akitembelewa na wageni wowote?",

"Hapana.",

"Unajua kazi aliyokuwa akifanya Montana?",

"Yeye aliniambia anafanya kazi kwenye stesheni ya redio, lakini sikujua kama ni mtangazaji wa Faraja.",

"Alikuwa akienda kazini saa ngapi na kurudi saa ngapi?",

"Aliondoka saa kumi na mbili au saa moja asubuhi na kurudi saa tatu au saa nne usiku.",

"Siku zote, au mwezi uliopita tu?",

"Siku zote. Na ndiyo maana sikuona tofauti yoyote ya ratiba yake.",

"Mama Zai, una tabia ya kuingia kwenye vyumba vya wapangaji wako wakiwa wametoka?",

"M-mimi? Ha-hapana!", mama Zai alijitetea.

"Umesema kwa kawaida Montana alikuwa akiondoka saa kumi na mbili au saa moja asubuhi. Ripoti ya polisi inasema kwamba uliukuta mwili wake saa kumi asubuhi. Ni kweli?", Reuben aliuliza.

Mama Zai aliuma kucha kwa hofu. 

"Niambie ukweli.", Reuben aliendelea, "Kwanini ulikwenda mlangoni kwa Montana saa kumi asubuhi, ukabisha hodi na baada ya kuona hakuna jibu ukatumia funguo ya ziada na kufungua mlango wake? Naomba sababu.",

"Nilikuwa na wasiwasi.", alijibu mama Zai kwa sauti ya chini na yenye woga.

"Kwanini? Kwani alikuwa anaumwa?",

"Hapana.",

"Alionesha dalili za kujiua?",

"Hapana.",

"Sasa ni kwanini ulikwenda?",

"Kwasababu ya kelele nilizozisikia kutoka kwenye chumba chake.",

Reuben na Joy walitizamana kisha kurudisha macho yao kwa mama Zai.

"Kelele gani?", Reuben aliuliza,

"Usiku wa saa nane, nilisikia mabishano makubwa kutoka kwenye chumba cha Montana. Kuna muda nilisikia mtu anachapwa makofi. Nilihisi ni wezi, nikaogopa kutoka nje. Baadaye kukawa kimya. Nilivyojibanza dirishani kuchungulia niliona mtu akitoka kwenye chumba cha Montana.",

"Mtu gani? Unaweza kuniambia jinsia?",

"Mwanamke.", mama Zai alinong'ona, "Ni mwanamke.",

"Uliweza kumtambua?",

"H-hapana. Alivaa mavazi ya kumficha sura. Alivaa tracksuit kubwa nyeusi, raba na soksi za mikononi.",

"Sasa ulijuaje ni mwanamke.",

"Soksi yake moja ya mikononi ilikuwa imetoboka. Niliona kucha za bandia nyekundu. Pia mwondoko wake ulikuwa wa kidada. Ni mwanamke. Nina uhakika.",

"Mama Zai, kwanini hukuyasema haya yote kwa askari?",

"Niliogopa. Yule mwanamke aliniona nikichungulia dirishani. Alifika mlangoni kwangu na kuacha bunda la pesa kwenye ngazi.",

"Hizo pesa zipo wapi?",

Mama Zai alihofia kusema.

"Hilo bunda la pesa lipo wapi?", Reuben aliuliza tena,

"Lipo mbali.",

Reuben alitabasamu kidogo, "Mama Zai, najua unahisi amekupa hizo hela basi tu, lakini tafsiri inaweza kubadilika na kukufanya uonekane kuwa ulishirikiana nae kumuua Montana.",

"HAPANA!", mama Zai alipayuka, "Mimi sio muuaji.",

"Mama Zai, uliona sura ya muuaji au hukuiona?",

"Sikuiona. Naapia kwa Mungu.",

"Mama Zai, uongo hautakusaidia chochote. Roho ya marehemu inatangatanga na ni wewe pekee ndiye unaejua ukweli. Hautakuwa unasaidia jeshi la polisi tu, bali utaifanya roho ya Montana ipumzike.",

"Nasema ukweli. Kama ni hizo pesa mnazitaka, kesho nitazileta hapa ofisini kwako. Ninasema ukweli.",

"Ukiachana na kucha na nguo alizovaa, kitu gani kingine unaweza kuniambia kuhusu mtu uliyemuona?",

"Si-sikumbuki kitu kingine. Ilikuwa giza.",

"Najua unachofikiria kwenye akili yako. Unahisi ukimfichia siri atakulipa pesa nyingi zaidi. Naomba nikukumbushe tu kuwa tunaongelea muuaji, mtu aliyeweza kumuua Montana na kufanya ionekane kama Montana amejiua mwenyewe. Kama ulimuona ni bora useme, maana yupo anakuhesabia siku tu. Nyie sio marafiki.",

"Nakuahidi. Nikikumbuka kitu kingine chochote wewe ndo utakuwa wa kwanza kujua.",

Reuben aliamua mahojiano yaishie pale kwa muda. Askari alikuja kumsindikiza mama Zai nje. Alibaki Joy na Reuben. Joy alihifadhi maongezi aliyorekodi.

"Nini kinafata, detective?", aliuliza Joy,

Reuben aliangalia saa yake, "Kabla siku haijaisha kuna mtu mmoja lazima nimhoji.", alisema,

"Nani?",

"Mkurugenzi wa Faraja station, Bwana Rajabu.",

"Mama Zai je? Umemalizana nae?", 

"Bado. Uzoefu wangu unaniambia kuwa kuna kitu muhimu ananificha. Bila shaka Mama Zai aliiona sura ya muuaji na ndiye mtu wa kwanza atakaemtafua baada ya kutoka hapa. Kama sikosei, tayari alikwishamtaarifu huyo kipindi anakuja hapa.",

"Unashauri vipi? Tutume askari wamfatilie kisirisiri?",

"Hapana. Kwa sasa, twende Faraja station. Tunahitaji kufahamu tajiri aliyemtumia Montana.",

Joy na Reuben walinyanyuka na kuondoka pamoja.

***

Next chapter