webnovel

chapter 47

Usiku umeshakuwa ni mnene lakini nyumbani kwa Nzagamba hakuna aliyepata lepe la usingizi.Kila mtu anageuka tu alipo lala wakifumba macho Yao wanaona kiza na wakifungua pia wanaona kiza.Tulya anaendelea kugeuka kitandani kichwa kikiwa kimejaa mawazo,kifua chake kikiwa kizito kutokana na kubeba moyo uliojaa majonzi.

Anachokipitia ni mtihani mkubwa.Siku zote akili yake imekuwa ipo haraka kutatua matatizo yake akifikiria ile mipango yake yote ya kupangua wachumba waliokuwa wanakuja nyumbani kwa Mzee Kijoola pasipo kutoa jasho,akitoka hapo anajipongeza kwa kuwa na wepesi wa kufikiria lakini Leo hii amekubali kuwa alichokuwa anakifanya hapo mwanzo alikuwa anacheza kwani hayo hayakuwa matatizo ya kuhitaji utatuzi ila hili la Leo ndio linahitaji utatuzi na limemfanya ajue uwezo wake wa kufikiria sio kama alivyokuwa anausifia.

Mawazo yake yanarudi masaa yaliyopita akiwa sebuleni kabla hajaja kuweka mwili wake kwenye kitanda chake kwa lengo la kulala wakati usingizi wake ukiwa bado unacheza kombolela unakojua wenyewe.

Baada ya swali la Nzagamba Tulya anaendelea kusimama asijue asemeje,hawezi kumwangalia kwani yeye mwenyewe hajui afanye nini? mambo yamekuja haraka kiasi kwamba akili yake yote imeganda.Siku zote amekuwa akitamani na kutarajia Nzagamba Kuja kwake na kumweleza hisia zake apate kumshauri na kumpatia nguvu,faraja na kumwambia yupo hapa kwa ajili yake lakini hakujua kama ombi lake lingejibiwa kwa njia ngumu namna hii,atamwambia nini?tayari ameshakuja na Yuko Mbele yake akimhitaji lakini hajui Cha kufanya,mkosi gani huu uliomkuta anawaza Tulya.

" Nitafanya nini?" anaisikia tena sauti ya Nzagamba anajikuta akivuta pumzi ya kutetemeka pasipokujua.Hana nguvu ya kugeuka na kumwangalia kwani anauhakika atalia tena msiba mkubwa na hataki kuonekana dhaifu kiasi hicho.

" umesema umechoka,pumzika" ndicho alichomjibu na pasipokugeuka kumwangalia alipiga hatua za haraka na kupotelea chumbani.

Kwa Sasa akiwa amelala anawaza Nzagamba atakuwa amejisikiaje kwa alichokifanya lakini alikuwa Hana namna anavuta pumzi ndefu na kuitoa anageuka pale kitandani na kulalia ubavu wake anafumba macho akiomba kesho kukipambazuka hii yote iwe ni ndoto kama ile ya Ndesha anayoiotaga Kila siku.

Kuna pambazuka Tulya anaamka na kukaa kitandani anafikicha macho yake anapiga mwayo na kuangalia huku na kule Kisha akili yake inajirudia yaliyotokea jana na kujikuta bado yupo katika mikono ya jinamizi linalomwandama.Asitake kupoteza mda miguu yake inatua chini anasimama na kujitengeneza vizuri nguo zake na kutoka chumbani,sebuleni anamuona Nzagamba akiwa bado amelala anamwangalia kwa mda Kisha kutoka nje.

Baada tu ya kufunga mlango mtu aliyekuwa amelala sebuleni anafungua macho yake anavuta pumzi na kutoa anaamka na kukaa mkono wake ukienda kichwani na kuzivuruga nywele zake zilizojisokota haamini kuwa anapitia mtihani ule tena baada ya watu kuanza kusahau na yeye akili yake iliyokuwa ikitawaliwa na kitu kingine kwa sasa mpaka kujisahau udhaifu wake laana yake inaamua Kuja kumkumbusha kuwa wao ni ndugu wa damu wanaotembea ndani ya mwili Mmoja na kuchangia mpaka kivuli Cha mwili wao inakuwaje anamsahau na kuamua kwendelea Mbele pasipo yeye na Sasa kuamua kumuadhibu kwa kumkumbusha ile aibu Yao ya milele.

" Nzagamba kaenda wapi mama?" Tulya anamuuliza Bibi sumbo aliyekaa chini ya mti akishona ukili.

Baada ya kurudi kutoka mtoni asimuone mume wake,wamepata kifungua kinywa yeye tu na Bibi sumbo tu mwanzoni alijua labda hajaenda mbali lakini mda umeenda jua limepanda juu na kuwa sio la kuvumilika tena na Nzagamba hajarudi.

" kwani hajakuaga?" Bibi sumbo anamuuliza akiendelea kushona ukili wake.

" ndio,nilijua hajaenda mbali atarudi,kaenda mtoni au?" anamuuliza.

" mmmmhhh," Bibi sumbo anavuta pumzi akiacha kushona ukili wake na kumwangalia mkamwana wake.

" kulikoni mama?"

" ulivyotoka tu na yeye akabeba silaha zake,naona atakuwa kaenda kuzifanyia mazoezi?" Bibi sumbo anamjibu.

" nini?" Tulya anauliza macho yakiwa yamemtoka.

" ndio,sijamuona siku nyingi akiwa amebeba silaha, mmmmhhh mwanangu sijui anawaza nini?"

" anafanyia wapi mazoezi?"

"ukienda kama unaelekea mtoni ukifika njia panda pale Mbele kidogo si unakionga kinjia kidogo kimeingia kushoto?"

" ndio"

" basi ingia na hicho kinjia Mbele utakuta Kuna mti wa mkuyu mkubwa utamkuta Nina uhakika" Bibi sumbo anamwelekeza.Tulya anapiga hatua za haraka kuelekea ndani akimwacha Bibi sumbo akimwangalia kama kachanganyikiwa au kafikishiwa habari mbaya.

kwa Sasa Tulya Yuko njiani baada ya kubeba kikapu Cha chakula na kibuyu kidogo Cha maji akielekea aliko Nzagamba uso wake ukiwa na tabasamu.

Anakaribia eneo la mkuyu anamuona Nzagamba akiwa anafanya mazoezi ya mishale Tulya anaongeza kasi ya hatua zake kiasi kwamba angekuwa na mabawa angepaaa awahi kufika.Anafika na kwenda chini ya mti kwenye kivuli anaweka kikapu chake na kibuyu anasimama na kuanza kumwangalia Nzagamba akilenga mishale yake kwa ufasaha pasipo kukosa alama.

" ni imara kuliko nilivyofikiria" anawaza akimwangalia Nzagamba aliyekuwa hajua uwepo wake pale.

" njoo upumzike ule unywe na maji" Nzagamba anashtuliwa na sauti nyuma yake anageuka na kumwona Tulya kwenye kivuli akimwangalia uso wake ukiwa na tabasamu.

Anamwangalia kwa mda asijue amefika saa ngapi anageuka na kuendelea na kazi yake.Tulya anaamua kumfuata baada ya kuona anampuuzia.

" Nzagamba jua limeanza kuwa Kali njoo huku up....aahhh!!" Nzagamba anageuka na kumuona Tulya akiwa chini sio mbali na alipo anatupa upinde wake chini na kupiga hatua haraka na kufika alipo " upo sawa?!" anamuuliza akiinama na kumwangalia Tulya akipapasa goti lake.Alikuwa anatembea macho yote kwa Nzagamba asione kisiki na kikampeleka chini.

" sio mbaya" anamjibu akijaribu kusimama Nzagamba anamsaidia " pumbavu kisiki hiki" Tulya anatukana baada ya kuona kile kilichomuangusha Nzagamba anatabasamu.

" wewe ndio hukutembea kwa uangalifu" Nzagamba anamjibu wakianza kutembea kuelekea kivulini.

" unatetea kisiki au?" anamuuliza Nzagamba asijue cha kumjibu zaidi kucheka kwa ndani.

" kaaa hapo" anamwambia na kutaka kugeuka kuelekea alipokuwa Tulya anamshika mkono.

" hujala kifungua kinywa na Sasa mda umeenda wa kupata Cha mchana kula ndio uendelee"

" Sina njaa" anamjibu na kutaka kuondoka tena.

" kula hujala tangu Jana,kaaa" anamlazimisha kukaa kwenye gogo la mti anamtengea chakula na kumnawisha Nzagamba Hana chaguo nakuanza kula.kimya kinapita kati yao zaidi ya sauti ya meno ya Nzagamba yakitafuna chakula.

" mmmh" Tulya anakohoa kidogo na kufanya Nzagamba kumwangalia.

" uko vizuri kulenga mishale umeanza kujifunza tangu lini?" anamuuliza akiangalia ubao uliojaa mishale aliyolenga Nzagamba pasipo kukosa.

"tangu Nina miaka nane,baba yangu alinifundisha" anamjibu macho yake yakienda kwenye ubao.

" lete nikusaidie" Tulya anashika kibuyu baada ya kuona Nzagamba kamaliza kula na kutaka Kunawa.

" acha tu,najiweza" anamjibu na Tulya kurudisha mkono wake.kimya kinapita kati yao tena.

"hujutii uamuzi wako tena?" Nzagamba anavunja ukimya.

" uamuzi gani?" Tulya anamuuliza macho yake yakimwangalia Nzagamba anayeangalia Mbele.

" wa kuolewa na Mimi" anajibu na kumfanya Tulya amwangalie kwa mshangao akijiuliza ni kipi kimemfanya afikirie hivyo.

" kwa nini unasema hivyo?" anamuuliza Nzagamba anatulia kidogo ulimi wake unatoka na kulamba mdomo wake kama chakula kilikuwa kitamu sana.

" nikaona kuwa huu ndio muda muafaka wa kukimbia au kuanza kujutia kuolewa na mtu kama Mimi"

Tulya anameza funda la mate akiona ni jinsi gani Lindiwe kumuacha Nzagamba kulivyo mwathiri mda wote anawaza kuwa watu watamkimbia isipokuwa mama yake kwa sababu ni mwanae hivyo hawezi kumtelekeza.

" kwani wewe una matatizo gani?"

anamuuliza Nzagamba anageuka na kumwangalia macho Yao yanakutana.

" huna tatizo lolote Nzagamba,Kila mtu anamapungufu yake hapa duniani,wengine yamejificha na wengine yanaonekana,wengine makubwa na wengine madogo isipokuwa Kuna ya wengine ambayo huwa yanasimama kama dole gumba kati ya vidole vya mikono au miguu,je utalitoa dole gumba mkononi mwako kwa sababu ni kubwa kuliko vingine au utatoa kadogoo sababu ni kadogo kuliko vingine?" anamuuliza na kutulia kidogo kama anasubiri jibu na kuendelea.

" hapana si ndio?" anamuuliza tena.

" dole gumba linaweza kuwa kubwa kuliko vingine lakini sio kama halina thamani kwani linakamilisha uwiano wa vidole vitano kisipokuwepo hiyo nayo inakuwa kasoro,ndivyo tulivyo binadamu tunatofautiana kama vidole vyetu hivi" anaongea akiangalia vidole na Nzagamba akimwangalia na kumsikiliza kwa makini.

" Kila kidole kina kazi yake,kikiondoka kimoja Kunakuwa na mapungu,pamoja na kutokulingana kwao kimo bado vinategemeana,udhaifu wako hujakufanya usiwe na thamani katika nyanja zote za maisha,kuwinda unaweza kuwa huwezi lakini unaweza kumtega ndege na kufanya kazi zingine na katika udhaifu wa mtu ndipo unapokuja uhitaji wa mtu wa pili Ili kuziba pengo hilo" anatulia kidogo na kushika mkono wake akimwangalia usoni

"katika udhaifu wako nipo Mimi kuziba ufa huo na Ili kuzuia mpasuko usiendelee kwa hiyo usiseme hujakamilika kwani katika pengo lako nipo Mimi kukutafunia nyama ngumu umeze" anaongea nakufanya mapigo ya moyo wa Nzagamba kuongea kasi faraja ikimjaa moyoni " na usifikirie tena kuwa ipo siku kuwa nitakukimbia,nilishakwambia kuwa nimekuja nikiwa nimebeba Kila kitu kwetu,siku zote utaniona nikiwa pembeni yako unachotakiwa kufanya ni kugeuza shingo yako kidogo tu na utaniona, unaponihitaji nitapiga hatua haraka na kufika ulipo"

" mbona ulikimbia?" Nzagamba anamuuliza na Tulya kumwangalia kwa mshtuko.

" lini?"

" Jana usiku"

kumbe alitambua hilo anawaza Tulya akijiuliza kama alimuumiza kwani hakuwa na lengo hilo hata kidogo.