webnovel

chapter 2

kiza kimetanda,nyota zimejianika kwenye zulia jeusi zikiangaza mwanga hafifu, tulya na mama yake zunde wakiwa bado wanachanja mbuga kuelekea himaya ya mpuli kwa mbali wanakaribishwa na mwanga wa miale ya moto ikiwa imewaka katika nyumba mbali mbali Kijijini.

Tone la matumaini linamdondokea tulya baada ya kuona Kijiji kwa mbali akiwa kwenye kilima akiiangalia himaya kwa chini,anavuta pumzi ndefu ya kujipa hongera kwa mwendo alioupiga kuanzia asubuhi,tumbo likiunguruma kuashiria linahitaji chakula na Koo kuashiria linahitaji maji,anaangalia Kijiji na kuona kinapendeza sana usiku huu angetamani angekiona mchana.

Himaya ya mpuli iliyozungukwa na milima na mabonde mengi yaliyosababisha kuwa na mito mingi na mapori yakutosha kuwa na wanyama wengi, kumefanya wakazi wa himaya hii kuishi kwa kuwinda na kula nyama za wanyama pori, hicho ndio kipato Chao kikubwa na kama wakihitaji vitu vingine watahitajika kuwinda wanyama na kwenda kufanya biashara ya mabadilishano na himaya zingine zinazojishughulisha na shughuli zingine kama ufugaji na kilimo kuendeleza mahitaji yao.

Tulya anamkimbilia mama yake ambaye alikuwa ametangulia kwa hatua kama tano akimwacha nyuma pindi alipokuwa akiichunguza himaya ya mpuli na kujiuliza maswali kuwa ataishi hapa kwa mda gani Ili arudi nyumbani kwao.

Wanaendelea kutembea mpaka Wanaingia ndani ya Kijiji na kuanza kukutana na nyumba mbalimbali,Kijiji kilikuwa kimya kuashiria kwamba watu wote walikuwa wamelala mda mrefu na kwa muda huu kwao ni kama usiku wa manane.

Tulya alikuwa akijipa moyo kuwa labda nyumba inayofuata ndio hiyo lakini wapi mda ulizidi kuyoyoma na safari ikawa ndo kwanza inaanza kupamba moto,hapo ndo tulya anakuja kukumbuka mama yake alikuwa akimwambia kuwa himaya Yao Iko mbali mtu anatakiwa kutembea kwa siku mbili ndio afike huko akiwa anapumzika njiani,au anaweza kutumia siku Moja na nusu asipopumzika na wao wameanza kutembea tangu asubuhi pasipo hata kukaa jua lote la mchana lilikuwa lao ndio maana baada ya kuona miale ya moto alipata matumaini kuwa wamefika lakini tumaini hilo linaingia mchanga.

Anatamani kulia lakini anajua kabisa hiyo haitasaidia na itamfanya mama yake kurudi kwenye maada yake ile aliyotembea nayo siku nzima,hivo anaamua kunyamaza na kuendelea kumfuata mama yake.

Baada ya mwendo wa kama masaa matatu uvumilivu unamshinda tulya "mama bado tu kama bado sana kwa nini tusitafute Mahali tulale tuendelee kesho" zunde hamjibu mwanae chochote anaendelea kutembea tu,tulya anaanza kuzolota nyuma lakini hiyo haikuchukua hata mda mrefu baada ya kupita nyumba Moja na kukimbizwa na mbwa anatoka mbio kama sio yule ambaye ungemwambia kimbia nikupe zawadi angekuona una pembe mbili kichwani na masikio kama ya punda.

Mbio hizo zinamfanya zunde acheke pasipo kugeuka nyuma kumwangalia mwanae "hivi mama ilikuwaje ukaolewa na baba"tulya aliuliza swali ambalo limekuwa likimsumbua tangu aichoke safari hii "mapenzi hayana mimpaka wala umbali mwanangu kama miungu imepanga mkutane mtakutana tu"

Tulya anamshangaa mama yake kwa kauli yake na ubongo wake ukimuuliza kwa mapenzi gani wakati ameolewa mke wa tatu.

Lakini ukweli unabaki kuwa palepale,kumbukumbu zikipita zikipita kichwani kwa zunde namna alivyokutana na mumewe.

zunde alikutana na Mzee kijoola katika Moja ya minada ya mabadilishano ya bidhaa,zunde akiwa amepeleka nyama ya swala kubadilisha apate maziwa akiwa ametumwa na baba yake aliyekuwa anapenda sana maziwa.

Akiwa huko alipata shida sana kupata maziwa sababu watu wengi waliokuwa wakibadili maziwa walikuwa hawataki nyama,Mzee kijoola aliyemuona zunde akihangaika kwa mda mrefu alimfuata "kwani unataka kubadilisha na nini dada" zunde alishtuka kusikia sauti nyuma yake anageuka na kukutana na mwanaume mrefu aliyekuwa na kifua kilichojazia vizuri,misuli yake ikiwa imemkaa vizuri kabisa na kumuangalia usoni alikuwa ni mzuri kweli.

Zunde alipata wakati mgumu kujirudu na kubaki akimwangalia tu kijana huyo,kijoola baada ya kuona binti kazubaa aliachia tabasamu lililomfanya zunde kuchanganyikiwa zaidi "nakuuliza unataka kubadilisha nini?" kijoola aliamua kurudia swali tena hapo ndipo zunde alipoamka kwenye ndoto yake ya mchana na kujikakamua kujibu"Nina nyama ya swala nataka maziwa lakini watu wamaziwa wote hawataki nyama" kijoola anamwangalia zunde kwa mda Kisha anageuka nyuma yake "niangalizie huyo mbuzi hapo nakuja mara Moja"alimwambia kijana mwenzake na kumgeukia zunde "nifuate huku"zunde anamfuata kijoola nyumanyuma na akafika sehemu akasimama na kuanza kuongea na Mzee Mmoja wa makamo "bado una maziwa"aliuliza kijoola,Mzee anwangalia kijoola "ndio unanjaa kiongozi" Mzee anamtupia kijana swali huku akichukua kipeo kilichokuwa karibu yake akikisafisha lakini alikatishwa na kijoola "hapana Mzee" Mzee anarudisha kipeo chake na kubaki akimwangalia kijoola kwa uso wa maswali kuona hivi kijoola anaendelea "naomba umfanyie msaada wa kumbadilishia maziwa huyu Binti" anaongea kijoola akimnyoshea mkono zunde.

Mzee anamwangalia zunde na uso wake ukaonyesha ishara ya kumtambua "hapana huyo ananyama ya swala na Mimi sihitaji nyama leo" anajibu Mzee akiyageuzia macho yake kwa kijoola "mpatie bwana hutapungukiwa chochote utaenda kula mchuzi mzuri wa swala shida Iko wapi" alibembembeleza kijoola "haya sababu umesema wewe nitakukataliaje wakati najua njiani narudi na wewe,lete kibuyu hicho Binti"

Zunde alipata maziwa kwa msaada wa kijoola "asante kaka" zunde alimshukuru kijoola baada ya kuondoka Mahali pale "usiwe na wasiwasi dada huo ni msaada tu,naitwa kijoola wewe je?" kijoola alijitambulisha "zunde"zunde naye alitaja jina "haya karibu,nilikuja kubadilisha mbuzi naona sina bahati Leo" zunde anamwangalia kijoola nakumwonea huruma kwani anajua wanatoka mbali kurudi na mzigo tena inakuwa shida lakini alikuwa hana Cha kumsaidia.

Wanaagana na zunde anaondoka kabla hajafika mbali anakutana na Mmoja wa rafiki wa baba yake Mzee lingo "shikamoo mjomba" anamsalimia kwa heshima akiukunja mguu wake wa kushoto Hali iliyomfanya ainame kidogo kwa kuonyesha heshima" Marhaba Mwanangu hujambo" anaitikia Mzee lingo huku akimwangalia zunde akiwa na kibuyu" naona ulifuata maziwa ya baba yako" "ndio"anajibu zunde huku macho yake yakitua kwenye kibuyu alichobeba "na wewe mjomba" anamuuliza swali huku akimdadisi "nimekuja kutafuta mbuzi nabadilisha na ngozi ya dubu"anajibu Mzee lingo akionyesha ngozi yake uliyokuwa mgongoni pake ambayo zunde hakuiona hapo mwanzo kutokana na kaniki yake aliyoijifunika.

Zunde akili inamcheza haraka "njoo huku mjomba Kuna sehemu nimeona mbuzi aliyenona"anaanza kutembea na Mzee lingo anamfuata nyuma anafika mpaka aliposimama kijoola "huyu hapa mjomba" kijoola aliyekuwa akiongea na mwenzake anashtushwa na sauti ya zunde anageuka na kumwangalia anamuona akiwa na Mzee "kweli amenona,unabadili na nini kijana"anaongea Mzee lingo huku macho yake yakiondoka kumwangalia mbuzi na kwenda kwa kijana "ngozi nzuri tu Mzee"anajibu kijoola kwa adabu "basi umepata mjomba anangozi nzuri ya dubu,hiyo ni maridadi sana kutengeneza kaniki"anaongea zunde huku macho yake yakijaa furaha ya kuweza kumsaidia kijoola "basi nitachukua hiyo Mzee" anajibu kijoola huku akimwangalia zunde kwa tabasamu na jicho la kumshukuru kitendo hiki kinamfanya zunde aangalie chini akichezea kuvha zake akizuia mapigo yake ya moyo yasisikike maana yalikuwa yakipiga hodi kifua kwa fujo.

Mzee lingo anaweka ngozi yake aliyobeba chini kijoola anaikagua na kuridhika nayo.wanabadilishana na zunde na Mzee lingo wanaanza kuondoka huku zunde akigeuka mara kwa mara akimwangalia kijoola anayempatia tabasamu la kwa heri.

Mazoea yaliongezeka kati ya zunde na kijoola Kila ilipofika siku ya mabadilishano zunde alienda na wakati mwingine kumpelekea chakula kijoola badae zunde alikuja kujua kuwa kijoola alikuwa kiongozi wa msafara wa wabadili bidhaa waliokuwa wakitoka katika himaya ya kinambu walikokuwa wakitokea wafugaji ndio maana Kila siku ya kubadilisha bidhaa alikuwepo hata kama yeye alikuwa Hana Cha kubadili ilimbidi afike na kuwasaidia watu wake kubadili bidhaa alifanya Kila kitu Ili watu wake wasirudi na bidhaa zai nyumbani.

Taratibu mapenzi Yao yalishamiri na kijoola aliamua kupeleka posa nyumbani kwa kina zunde awali baba yake zunde na kaka yake walikataa kwa sababu mbalimbali,kwanza zunde alikuwa bado mdogo alikuwa hajaingia hata mafunzo ya mwali,pili mwanaume aliyekuwa anataka kumuoa tayari alishaoa akiwa na wake wawili akimzidi umri umbali mrefu,tatu alikuwa anatoka mbali sana hawakutaka kumtupa mtoto wao mbali kiasi hicho na walijua kuonana nae ingekuwa kwa shida pindi akiolewa, na mwisho kulikuwa na posa zingine nyingi kutokana na urembo wa zunde wanaume wengi pale Kijijini walimtaka hivo waliona Haina haja ya kumuozesha huko.

Lakini zunde aling'ang'ania na kusema anampenda kijoola ataolewa nae hivohivo,baada ya marumbano ya mda mrefu ikabidi wakubali zunde akatolewa mahari akaingia mafunzo ya mwali na baada tu ya kumaliza alikuja kuchukuliwa na kijoola akiwa mke halali wa tatu,licha ya wake wenza kumnyanyasa kutoka na wivu zunde anavumilia akijua kijoola anampenda mpaka dakika ya mwisho.Zunde anatabasamu akimalizia kumbukumbu za mapenzi yake ya ujana na Mzee kijoola.

Zunde anasimama Mbele ya nyumba nnee zilizozungukwa na miti mirefu akiangalia huku na kule,mbwa baada ya kuona harufu ngeni na watu wakiwa wamesimama nje ya zizi wanaanza kubweka,tulya anajificha mgongoni kwa mama yake "hodi!hodi!hodi!" anaita nzunde kwa tahadhari.

Wanakaa kwa mda bila majibu na zunde anarudia tena "hodi!wenyewe humo ndani"safari hii sauti ikiwa juu kidogo akitaka mtu aliyeko ndani amsikie kwa sababu ingekuwa ni vigumu kutoka na mbwa waliokuwa wakifanya kazi Yao ya ulinzi kwa ustadi mkubwa,baada ya muda mlango unafunguliwa."nani huyo" inasikika sauti ya mtu aliyetaka ndani ikionyesha dhahiri ametoka katika usingizi mnene.

Zunde anasogea karibu kidogo "samahani kwa kukuamsha na kukusumbua Mimi ni mgeni maeneo haya nilikuwa naulizia kwa Mzee Matiko mwanae anaitwa Shani matiko" anauliza zunde.tulya anabaki mdomo wazi akimshangaa mama yake kuwa hapajui kwao.