webnovel

chapter 22

Nzagamba anaangalia familia ya bibi harusi wakifika wakiwa na Tulya aliyekuwa amefunikwa kaniki usoni na watu wengine wakicheza akiwemo sinde na mama yake.

" shemeji yetu huyo kaingia" anasikika Mkita akiongea aliyekuwa pembeni ya Nzagamba akiwa na washawasha ya sherehe kama anaoa yeye,upande mwingine akisimama Lingo na Ntula.

Nzagamba anamwangalia mama yake bibi sumbo akicheza akiwa na furaha usoni ambayo hajawahi kuiona kwa mda mrefu sana,roho yake inapata amani akijua hata kama ndoa haina upendo angalau imeleta tumaini kwa mama yake hivyo anapata faida mojawapo ya kumuoa Tulya.Akiwa kwenye msongo wa mawazo anashtuliwa na sauti ya Mkita iliyokuwa kama zeze siku ya Leo.

" wanamfungua"

Macho yake anayatoa kwa mama yake na kuyaelekeza kwa Tulya na kumuona shangazi yake akimsogelea na kushika kaniki iliyokuwa kichwani kwake na kuitoa,ndirimo na vifijo zikasikika watu wote wakishangilia na kupiga vigelegele na nyimbo za kumsifia bibi harusi zikipigwa.

Lakini hayo yote Nzagamba alikuwa hayasikii wala hao watu waliokuwa wakicheza alikuwa hawaoni,macho yake yalikuwa yametua kwa tulya yakimtathimini kwani hakuamini kumuona akiwa amependeza namna ile,muda huo tulya akiwa ameinamisha kichwa chini kama bibi harusi mtiifu lakini Hali hiyo ilikuwa inamkosesha Nzagamba uvumilivu aliyekuwa anasubiria kuiona sura yake,sio yeye tu watu wote waliokuwa eneo hilo walikuwa na wazo hilo.

Nzagamba maombi yake yanajibiwa kwani sio mda mrefu anamuona Tulya akinyanyua sura yake na kuangaza huku na kule mpaka macho yao yalipokutana.mapigo ya moyo wa Nzagamba yanapoteza hesabu kwani yanatulia kwa muda kabla ya kuanza safari Yao ya kusafirisha damu mwilini.

Nzagamba anamwangalia Tulya kama ni msichana tofauti aliyekutana nae siku kadhaa nyuma.Ingawa hakumuona mara nyingi alijua kuwa alikuwa ni wa kuvutia lakini ukweli ni kuwa Leo anamuona ni wa kuvutia sana.

" ni mrembo sana" maneno hayo yanamchomoka mdomoni pasipo yeye kujua.

"umekwisha Nzagamba" mkita aliyekuwa kwenye mshtuko sambamba na wenzake hakuweza kufunga mdomo wake.

"nini tena hiyo" anaongea ntula baada ya kumuona Tulya akirudisha uso wake chini tena sura yake ikionyesha kukereka kwani bado alikuwa anataka kumwangalia vizuri.

" kuweni na adabu ni shemeji yenu huyo" anaongea Lingo kuwarudisha kundini wenzake .

" lakini ni mzuri sana ndio maana alikuwa gumzo mtaani,hata Nzagamba hakulijua hilo, unamuona alivyobadilika?" Mkita asiyejua kuacha Mambo yaende anaongea na kuwafanya wenzake wote kumwangalia Nzagamba aliyemeza funda kubwa la mate na kuanza kujitahidi kurudi maeneo yale.

"Mimi mwenyewe nimeshtuka,mshtuko wake utakuwa mkubwa zaidi" Ntula anaongezea na kufanya Nzagamba kumkata jicho la funga mdomo wako.

Kwa upande wa Tulya alitakiwa kuwa bibi harusi mtiifu asiyeangalia watu usoni, lakini shauku ya kumuona Nzagamba ikashinda mafunzo ya Somo wake.Ananyanyua uso wake taratibu na kuanza kuangalia Mahali alipo Nzagamba na haikuchukua muda mrefu kumuona akiwa amesimama upande wa pili kutoka Mahali alipokuwa.

Macho yake yanatua kwake kwa muda na kumuona Leo ambavyo anaonekana tofauti kidogo,akiwa amevalia rubega yake na kiunoni akiwa amefunga mshipi.Pembeni ya kiuno chake akiweka sime yake ambaye mara nyingi huwezi kumuona akiwa na silaha na kwa sababu Leo ni siku ya harusi yake ndio maana ameibeba kwani ni tamaduni,macho yake yanarudi juu usoni kwake kumwangalia na kuona sikioni kwake akiwa amevaa jaribosi kubwa ya kuning'inia.

macho yao yanapokutana Tulya anawahi na kuficha sura yake kwa kuinamisha uso wake asije akainekane bibi harusi ambaye hakuwa na woga anayemkodolea macho mumewe mtarajiwa.Lakini hakujua kitendo kile kilimfanya Nzagamba aachiye tusi kimoyomoyo kwani alikuwa bado anataka aendelee kuangalia sura ya Tulya.

" mbona mzuri hivyo imekuwaje kaamua kujitoa kafara namna hii huyu Binti" Tulya anasikia sauti ya mwanamke akiongea umbali kidogo na aliposimama

" Mimi mwenyewe nashangaa,kwa mwanamke kama huyu angeolewa hata na mtemi au tajiri yeyote kwa mahari kubwa kabisa" anasikika mwingine.

" ndio,Sasa imekuwaje kajitutumua namna hii,au kaponzwa na utanashati wa Nzagamba asijue madhara yake?" anaongea yule wa kwanza akimuuliza mwenzie swali.na mwenzake anamjibu kwa kusema.

" kwa nini asijue wakati hata mpita njia muomba maji anapata habari itakuwa yeye,nasikia kakaa miezi kadhaa hapa Kijijini hivyo nina hakika habari anayo"

" kwani nyie hamjasikia kuwa alitakiwa aolewe na Manumbu akakataa,ndio akachagua kuolewa na Nzagamba" anadakia mwingine akiwapasha wenzake nyepesinyepesi zilizowapita Kijijini.

" mizimu ya ukoo wangu walahi huyu dada kajipotezea bahati" anasika Mmoja kati ya wale wawili wa awali akiita mizimu ya ukoo wake ije kumshuhudia.kitendo kilichofanya Tulya kukosa uvumilivu na kunyanyua sura kidogo awaangalie.

' harusi yangu,unaita mizimu ya kwenu hapa ya nini,hamuwezi tu kufunga midomo yenu mkaacha Mambo yakapita,msubirie sherehe iishe mle makande muondoke,na mkila makande naomba mkavimbiwe msilale usiku kucha mkae mlango wa choo' anawakaani kimoyomoyo.

Na wanawake wale wanaendelea na umbea wao wa kujadili hadithi ya mapenzi kati ya Nzagamba, Manumbu na Tulya,wakiongezea na chumvi Ili hadithi ipate radha.

Tulya anatupa mishale pale aliposimama hasira zikimpanda kwa watu wasiopenda furaha za wengine.Akiwaona wanabahati kiasi gani kwani yeye ni bibi harusi siku ya Leo,la sivyo asingewaacha kabisa.

Mlorongo wa mawazo na hasira yake inakatishwa na shangazi yake aliyemwambia asogee mbele huku watu wote waliokuwa Mahali pale wakiwa wamekaa kimya wakisubiri ukamilisho wa ndoa hii.

Anapiga hatua Mbele na kwenda kukaa kwenye ngozi iliyokuwa imetandikwa na Nzagamba akija kukaa pembeni yake.mapigo ya moyo yakimwenda kasi kwa ukaribu waliyokuwa wamekaa.

Mganga wa Kijiji anakuja na kusimama Mbele Yao akiwa na unyoya wa mkia wa nyumbu mkono mwake,anapitisha unyoya huo vichwani mwao akiwagusa.

Anaenda Mbele kidogo na kusimama,kijakazi wake anakuja na kibuyu kilichokuwa na pombe na kumpatia mganga huyo.mganga anakipokea na kumeza funda kubwa na kutema kwa kupulizia pande zote nne za Dunia huku mkono wake uliokuwa na manyoya ukiwa juu akiutupa kama anafukuza kitu Kila mara anapotema pombe hiyo.

Baada ya kumaliza kitendo hicho anampatia kijakazi wake kibuyu nae anakipokea na kuondoka pale mble.

" baba wa bibi harusi au mtu yeyote aliyepokea mahari aje hapa Mbele" anasikaka mganga na Mzee kijoola anasogea pale Mbele pasipokupoteza mda.

" umekubali kumuozesha Binti yako kwa Nzagamba?" mganga anamuuliza Mzee kijoola.

" ndio" Mzee kijoola anajibu akimwangalia Binti yake pale chini uso wake ukichanganyika huzuni na furaha.

" kwa mahari ipi mliokubaliana?" mganga anaendelea.

" kwa mahari ya mbuzi wa nne" anajibu Mzee kijoola safari hii macho yake yakiwa kwa mganga.

" umeipokea yote?"

" ndio"

mganga anamtupia mkono ishara ya kumuonyesha aondoke na Mzee kijoola anatii na kurudi nyuma na mganga anaendelea.

Anapiga hatua mpaka Mahali walipokuwa waamekaa Tulya na Nzagamba

"Nzagamba huyu ndiye msichana unayetakiwa kumuoa na uliyemtolea mahari ya mbuzi wa nne?"mganga anamuuliza Nzagamba.

Nzagamba anamwangalia tulya kidogo na Kisha kumwangalia mganga

" ndio,ni yeye"

" naiomba mizimu iwabariki wanandoa Hawa waliopo Mbele ya mizimu siku ya Leo,iwaondolee mikosi na mabalaa yote, iwapatie baraka nyingi za watoto na mali.iwaondoee mikosi yote itakayotupwa Mbele Yao" mganga anamaliza kuongea maneno yake na kijakazi wake anafika tena pale Mbele na kibuyu chake anampatia mganga naye anameza funda kama awali na kurudia kitendo kilekile Cha awali.

Baada ya kumaliza anaenda walipo maharusi na kusema " kuanzia Sasa nyingi ni mke na mume" watu wote wanapiga vigelele na ngoma,nyimbo,miruzi vikirudi tena kama awali chereko chereko zikiendelea.

Tulya na Nzagamba wanasimama Mahali walipokuwa wameka na kusogea pembeni mwa ngozi ile waliyokuwa wameikalia.Tulya anashtuka baada ya kuhisi mkono wa Nzagamba ukigusa wake kwa haraka ananyanyua sura yake na kumwangalia na macho yao yanakutana.

Tulya anarudisha uso chini na kukumbuka kuwa Sasa ni mda wa kushikana mikono.

' tulia Nzagamba haraka ya nini, kwanza kwa nini hataki kushikana mikono na Mimi?' anajiuliza baada ya kuona Tulya amesogeza mkono wake baada ya kumgusa akianza kuwaza labda ndio mda wa adhabu umeanza.

Lakini anashtushwa na kitendo Cha Tulya aliyeushika mkono wake na kuviunganisha vidole vyao.anageuza sura yake na kumwangalia Tulya na kukuta tayari anamwangalia kwa tabasamu huku akiendelea kuminya vidole vyao kiasi kwamba hata mtu akija kutoa hawezi labda akate na shoka.Kwa Tulya ilikuwa ni ishara ya kumuonyesha Nzagamba kuwa atakuwa na yeye wakati wote na kwa majira yote hata muacha kamwe.

'Huyu mwanamke ni kichaa haoni aibu kufanya hivi Mbele za watu' anawaza Nzagamba akiangalia pembeni kwani Nina uhakika angekuwa mweupe Sasa hivi angekuwa mwekundu kama nyanya kwa aibu.

' kwani unajua Leo,siku zote ni kichaa huyu' nafsi yake inamjibu na yeye kutikisa kichwa kukubaliana nayo, kitendo kilichoonekana na wengi pasipo yeye kujua.

Safari ya kuelekea eneo zinakofanyikiaga sherehe inaanza na maharusi wakitembea polepole huku watu wakiwa wamewazunguka pande zote njiani.

Baada ya kufika sehemu sherehe ilikokuwa inafanyikia watu wakiendelea kucheza wakapewa vyakula wakala na ngoma zikaebdelea tena.

Muda ulienda haraka hatimaye jioni ikawadia na ikawa ni muda wa maharusi kuondoka eneo hilo. " habari yako shemeji" Tulya anashtuliwa na kijana aliyekuja kuwasalimia akimpatia mkono ananyanyua uso wake na kuona vijana wengine wawili,anamwangalia Nzagamba Kisha kuupokea mkono " nzuri tu " anaitikia na kuutoa mkono wake.

"hongera sana,na karibu kwetu" anaongea mwingine " Tulya anatoa tabasamu na kuitikia "asante"

" nimeipenda suti yako ukweli kabisa" anaongea Mkita na kufanya kuambulia jicho Kali kutoka kwa Nzagamba lakini Mkita kama siku zote hajali hata kidogo " naitwa Mkita ni rafiki kipenzi wa Nzagamba"

" Nashukuru kukufahamu" Tulya anaitikia

" Na huyu hapa ni.."

Kabla hajaendelea Nzagamba anamkatisha

" Hawa marafiki zangu huyu ni Ntula,Lingo na Mkita" anamtambulisha na Tulya anawaangalia akitoa tabasamu.

' kwani ni kipaji chake kucheka au' anajiuliza Nzagamba baada ya kumuona Tulya akitabasamu jino kwa jino na marafiki zake.

" mnatakiwa kuondoka" anaongea Kilinge aliyefika hapo akiwa na Zinge.

" mmh" Nzagamba anaitikia akiwaangalia Zinge " siku nyingi hatujaonana Zinge"

" ndio ni siku nyingi,hongera na karibu kwenye familia" Zinge anamjibu akimpatia mkono.

" asante"

" ukimnyanyasa binamu yetu mrembo ujue kabisa hutabaki mpuli hii" Zinge anampa vitisho Nzagamba.

" usijali nimeshamwambia hilo" Kilinge anamjibu.

" wewe utamuonea huruma sababu rafiki yako lakini Mimi sitakuacha"

" usijali Zinge,nitamwangalia vizuri"

" msimtishe mwenzenu anamambo mengi ya kufanya,Leo ana usiku mrefu" baragumu mkita anawakatisha na kumfanya Tulya kuangalia chini kwa aibu na wengine wakicheka.

"ndio mnaondoka" anafika sinde akihema kama kakimbia maili mia njuga zake miguuni zikitoa sauti Kila akipiga hatua,kumbe kakosa pumzi kwa kucheza, anaongea na kuwaangalia wote.

"ndio" Tulya anaitikia na sinde anamkumbatia naye anarudisha kwa kuzungusha mikono yake mgongoni kwake.

"sijawaona kina mama muda mrefu?" Tulya anauliza akiangalia katikati ya watu kama atamuona mama yake

" wameondoka baada ya chakula tu" sinde anamjibu na hii inamuuma kidogo Tulya mama yake kuondoka tu pasipo kumuaga. sinde analiona hili.

" usijali watakuwa walikuwa wamechoka tu si unajua wamekuwa wakihangaika kwa siku kadhaa pasipo kupumzika,utaonana nao kesho wakati wa utambulisho"

Tulya anaitikia kwa kichwa "nitakumisi Sana na nitapozewa pia nilikuzoea sana" anaongea sinde machozi yakimlenga.

" si utakuja tu kunisalimia hapo sio mbali"

" najua,na usiku je nitalala na nani?"

" olewa na wewe acha kumzuga mwenzio" Ntula anamwambia.

" bado sana kama miezi mitatu hivi,mpaka Tinde atoke lindo" Lingo anajibu.

" acheni hadithi zenu hapa tuwaache waondoke,usiku mwema kwenu" anaongea Kilinge.

" sisi tunaenda" Nzagamba anaaga akimshika mkono Tulya na kuondoka Mahali pale kuelekea nyumbani kwao.

Ile wanafika karibu na mlango wa kuingia uani wanatokea wanaume sita na kusimama mlangoni kitendo Cha kuwashtua wote Tulya na Nzagamba.

" Ulidhani tutakuacha tu uondoke kwa ulichokifanya" anaongea mwanaume Mmoja kati Yao anayeonekana kama ni kiongozi wao.

" nyie ni kina nani?" anauliza Nzagamba kwani hajawahi kuwaona na Hana deni na mtu.

" sisi?hutujui sisi? kwa kosa ulilofanya la kuondoka na huyo halafu bado unajifanya hutujui sisi?"

"kaka lengi" anaita Tulya na Nzagamba kumwangalia kwa mshangao

" unawajua?" anamuuliza macho yake yakitoka kwa tulya na kwenda kwa wanaume wale.

"ndio,ni kaka zangu"

" wote Hawa?"

" ndio,na wengine hawapo"

Nzagamba akabaki anashangaa akiwaangalia kaka zake Tulya waliokuja kumvamia nyumbani kwake.

" Sasa umeshatujua sisi ni akina nani,ukimtesa mdogo wetu ujue hatutakuacha sawa?" anaongea yule mkubwa anayejulikana kwa jina la Lengi.

" kaka acheni kumtisha bwana" Tulya anamtetea mumewe.

" mwangalie kaka mapema hii ameanza kuwa upande wa mumewe" anadakia mdogo,Tulya anataka kuongea lakini Nzagamba anamkataza na kusema.

" msiwe na wasiwasi mdogo wenu atakuwa salama kabisa nawahakikishia"

Nzagamba kuongea vile moyo wa tulya unapata faraja isiyo na kifani akijua kuwa Nzagamba atamfanyia vyema hata kama hampendi.

" tutakuaminije sisi wakati tayari umeshatuonyesha rangi yako halisi"

" ehh!" Nzangamba anaitika asijue wanauzungumzia nini.

" Angalia umemtembeza mdogo wetu umbali wote huo kutoka kule wakati ulitakiwa umbebe" anauliza mwingine na Nzagamba kubaki Hana la kusema.

" sio hivyo kaka,alitaka kunibeba nikakataa Mimi" tulya anamtetea na Nzagamba kumwangalia kwa nini anasema uongo kwa ajili yake.

" samahani sana ni makosa yangu pasipo kufikiria vizuri"

" Sasa bado unasubiri nini?"

" ehh! sawa" Nzagamba anachuchumaa chini kuashiria ambebe Tulya.

' hiki Sasa kisanga Cha mashemeji' anajiwazia Nzagamba.

" kaka Haina shida tumeshafika" Tulya anakataa kwani hajisikii huru kubebwa na Nzagamba.

" ohhhh,usitake tumuadhibu Sasa hivi" anakemea kaka yake na tulya kukosa namna ila kupanda mgongoni kwa Nzagamba.

" haya nendeni,usiku mwema tutaonana kesho" kaka zake wanaaga na kutaka kuondoka.

" haya shemeji usiku mwema" nzagamba anawatakia usiku mwema na kuanza kutembea kuelekea ndani.

" Kila nikimwangalia,nahisi kama nimewahi kumuona Mahali" anaongea kaka mkubwa aliyekutana na Nzagamba Jana usiku wakati ameenda nyumbani kwa Mzee Shana.

" wapi ulimuona?" mwingine anauliza

" hata sijui"

" labda umemfananisha tu"

" labda"

' nashukuru mungu sikukaa nao mda mrefu Jana' anawaza Nzagamba baada ya kusikia mazungumzo yao akivuta pumzi ya ahueni na kuingia ndani.